Bwana Ban Ki-Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, akizungumza kwenye Baraza kuu
la Umoja wa Mataifa kuhusu ugonjwa wa Ebola, Jumanne tarehe 20 Januari 2015, amewapongeza
wadau mbali mbali ambao wamefanya kazi kubwa, usiku na mchana huko Afrika Magharibi
kwa ajili ya kuwahudumia waathirika wa ugonjwa wa Ebola na kwamba, wote hawa kwa hakika
wanapaswa kutambulikana kuwa ni mashujaa dhidi ya ugonjwa wa Ebola.
Changamoto
kubwa iliyoko mbele ya Jumuiya ya Kimataifa ni kuhakikisha kwamba, ugonjwa huu unadhibitiwa
kikamilifu na kupunguza athari zake kwa waathirika, jambo linalohitaji, ukweli na
uwazi.Jumuiya ya Kimataifa itaendelea kuwasaidia waathirika na kwamba, hadi sasa kuna
maendeleo makubwa, juhudi za ushirikiano na mfungamano wa kimataifa.
Jumuiya
ya Kimataifa kwa sasa anasema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa inaendelea kujielekeza
katika kutoa elimu na huduma za afya kwa waathirika, ili kuzuia na kudhibiti maambukizi
mapya na kwamba, nchi zilizoathirika kwa ugonjwa wa Ebola zinaanza kujiandaa ili kufungua
ukurasa mpya kwa kutoa huduma msingi kwa watu wake. Jumuiya ya Kimataifa haina budi
kuendelea kusaidia harakati za maboresho ya huduma muhimu pamoja na kuwasaidia watoto
yatima. Kuna haja ya kuwa na mikakati ya uhakika wa usalama wa chakula pamoja na kusaidia
mchakato wa wanafunzi kuanza kurudi tena shuleni, ili kuendelea na masomo.
Katibu
mkuu wa Umoja wa Mataifa anakiri kwamba, ugonjwa wa Ebola kwa hakika umetikisa nguvu
kazi, maisha, mapokeo, tamaduni na imani za watu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi
kuwekeza huko Afrika Magharibi, ili kuwaunganisha watu; kusaidia familia za wafanyakazi
waliopoteza maisha wakati wakiwahudumia wagonjwa wa Ebola pamoja na kuwawezesha watu
wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa waathirika wa ugonjwa wa Ebola.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.