2015-01-20 11:32:42

Papa Francisko kuwasha moto wa Injili Barani Afrika Novemba 2015


Baba Mtakatifu Francisko wakati akiwa njiani kurejea kutoka Manila, Ufilippini, Jumatatu tarehe 19 Januari 2015 amewaambia waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kwamba, anatarajia, Mungu akipenda kufanya hija ya kitume Barani Afrika kwa kutembelea Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na Uganda. Haya ni maeneo ambayo yamekuwa na mgogoro wa vita kwa miaka mingi na kwamba, kuna haja ya kuanzisha tena mchakato wa amani, upatanisho na mshikamano wa kitaifa.

Baba Mtakatifu anasema, panapomajaliwa, hija hii ya kitume inaweza kufanyika Mwezi Novemba, 2015, wakati ambapo hakuna mvua, ili aweze kupata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Familia ya Mungu katika nchi hizi. Baba Mtakatifu anasema, amekuwa na wazo la kutembelea Barani Afrika, lakini ilishindikana kutokana na kuibuka kwa ugonjwa wa Ebola, jambo ambalo lingegumisha mkusanyiko wa makundi makubwa ya watu.

Rais Yoweri Kaguta Museven alimpotembelea Baba Mtakatifu hivi karibuni, alipohojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kuhusu uwezekano wa Baba Mtakatifu Francisko kutembelea nchini Uganda kama sehemu ya mwendelezo wa maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu Mashahidi wa Uganda walipotangazwa kuwa Watakatifu, alisema, kwamba, Vatican itatangaza hija hii kwa wakati muafaka. Alisema, kwa mkazo kwamba, "Mambo ya wazee, wanazungumza wazee wenyewe".

Baba Mtakatifu Francisko amekwishafanya hija ya kichungaji Barani Asia mara mbili. Kuna mamillioni ya watu Barani Afrika yanateseka kutokana na umaskini, njaa, magonjwa, vita, kinzani za kijamii na mashambulizi yanayofanywa na watu wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani. Familia ya Mungu Barani Afrika inasubiri kwa hamu na matumaini makubwa kumpokea Baba Mtakatifu ili kuwasha tena moto wa Injili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.