2015-01-20 08:54:14

Mwaka wa maskini na Uinjilishaji Mpya!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini mara tu baada ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini humo, wameanza mara moja mkutano wao wa mwaka, ili kupembua kwa kina na mapana Uinjilishaji mpya pamoja na Maadhimisho ya Mwaka wa Maskini, kama sehemu ya mchakato wa Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 500 ya Ukristo nchini Ufilippini.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linaendelea kumshukuru Mungu kwa ujio wa Baba Mtakatifu Francisko ambao umewashangaza wengi na kwamba, changamoto alizowapatia ni kichocheo kikuu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu. Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanakiri, adhimisha, ungama na kumwilisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake katika uhalisia wa maisha, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa imani katika matendo.

Baba Mtakatifu alipokuwa nchini Ufilippini, Maaskofu wanasema, ameonesha dira na mwelekeo mpya wa Kanisa kuwajali na kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Maskini ni walimu wa tunu msingi za maisha ya binadamu, kwa kuonesha kwamba, mtu ni kwa jinsi alivyo na wala si kutokana na mali, utajiri au nafasi yake katika jamii. Watu wajifunze kuwa na imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu hasa pale wanapokosa majibu muafaka wa Fumbo la Mateso na Mahangaiko ya binadamu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linasema kwamba, Baba Mtakatifu ameiachia Familia ya Mungu nchini humo changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa, ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana.

Maaskofu wanampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, zinazokabiliwa na changamoto mamboleo. Amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema "kuwatolea uvivu" wale wanaokumbatia utamaduni wa kifo na badala yake, wasimame kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya Uhai na Familia, mintarafu tamaduni na mapokeo hai ya wananchi wa Ufilippini.







All the contents on this site are copyrighted ©.