Wakristo na Waislam hawana budi kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha kwanza
kwa mambo msingi yanayosaidia kujenga na kudumisha mshikamano na mfungamano wa kijamii;
kwa kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana; kila mwamini akijitahidi kushuhudia
utambulisho wake wa kidini na kitamaduni. Mauaji ya watu wasiokuwa na hatia pamoja
na uharibifu wa nyumba za Ibada ni matokeo ambayo kamwe hayawezi kuvumiliwa na wapenda
amani na utulivu. Si vyema watu kukashifiana katika dini na imani zao, kwani jambo
hili ni hatari kwa usalama, amani na utulivu wa kijamii.
Ni changamoto inayotolewa
na Askofu mkuu Claude Rault wa Jimbo Katoliki la Laghouat-Gardaia nchini Algeria kufuatia
kashfa za kidini ambazo zimeendelea kusababisha maafa na uharibifu mkubwa wa nyumba
za Ibada. Askofu Rault anasema, kuna haja kwa wamini wa dini mbali mbali kuheshimiana
kwa kutambua na kuendeleza tunu msingi zinazowaunganisha pamoja kama taifa sanjari
na kuendelea kujikita katika ujenzi wa jamii kwa kufanya kazi kwa bidii, juhudi na
maarifa; kwa kuzingatia misingi ya ukweli na uwazi, kila mtu akijitahidi kutekeleza
wajibu wake barabara.
Watu watambue kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano
wa Mungu. Mauaji ya watu wasiokuwa na hatia kwa kisingizio cha misimamo mikali ya
kidini na kiimani ni jambo ambalo linapaswa kukemea na wapenda amani wote. Watu wanategemeana
anasema Askofu Rault na hakuna mtu anayeweza kuishi kama kisiwa, jambo la msingi ni
kuheshimu dhamiri za watu, kutafuta na kudumisha mafao ya wengi sanjari na uhuru wa
kuabudu. Hapa kama anavyosema Baba Mtakatifu kuna haja ya watu kujenga na kuimarisha
madaraja ya watu kukutana na kusaidiana na wala kuta zinazowatenga watu kwa misingi
ya udini, ukabila na umajimbo. Uhuru wa kuabudu, upendo na mshikamano wa kidugu ni
mambo msingi katika kudumisha amani na utulivu wa kijamii.
Na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.