Athari za mabadiliko ya tabianchi ni tishio kwa maisha ya binadamu!
Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kwamba, mkutano wa ishirini
na moja wa Jumuiya ya Kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, unaotarajiwa kufanyika
Paris, Ufaransa Desemba, 2015, utaweza kufanya maamuzi machungu, ili kujenga na kuimarisha
umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya
tabia nci ambayo yanaendelea kuwa ni chanzo cha majanga kwa nchi nyingi duniani.
Ukuaji
wa mikakati ya kiuchumi si kigezo pekee cha maendeleo ya binadamu na kwamba, kuna
haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kushirikiana zaidi, ili kupambana na baa la
umaskini wa hali na kipato. Jumuiya ya Kimataifa ilikuwa imejiwekea Malengo ya Maendeleo
ya Millenia ifikapo mwaka 2015. Maaskofu wa Ufaransa wanasema, baadhi ya Malengo ya
Maendeleo ya Millenia yamefikiwa. Lakini baa la umaskini na njaa, ni kati ya mambo
ambayo hayana budi kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa, ili kulinda na kudumisha
utu na heshima ya binadamu. Kumbe, hapa kuna haja wanasema Maaskofu wa Ufaransa kujiwekea
malengo ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kukuza mikakati ya ukuaji
wa uchumi na maendeleo ya watu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa linasema,
Kanisa kwa upande wake, linapenda kuwapatia watu matumaini, kwa kukazia mafao ya wengi
yanayojikita katika mshikamano wa kimataifa. Ili kujenga matumaini, kuna haja ya kuwa
na mwelekeo mpya wa mtindo wa maisha katika masuala ya ulaji unaowajibisha katika
mchakato unaowawezesha watu kujitambua kwamba, wanahusika katika uzalishaji na utunzaji
bora wa mazingira.
Maaskofu Katoliki Ufaransa wanasema, kuna haja ya kusimama
kidete kulinda na kudumisha mafao ya wengi kwa kupambana kufa na kupona na athari
za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea kusababisha umaskini mkubwa kati ya watu.
Hapa kuna haja ya kuwa na sera na mikakati makini: kitaifa na kimataifa, kwa ajili
ya mafao ya wengi, kwa kuongozwa na kanuni auni inayojikita katika mshikamano, ili
kuwasaidia maskini kuondokana na umaskini wao. Ikumbukwe kwamba, hakuna mtu anayeweza
kujitosheleza binafsi, kumbe, kuna haja ya kusaidiana ili kupambana na umaskini kama
sehemu ya mchakato wa huduma kwa Familia ya binadamu.
Baraza la Maaskofu Katoliki
Ufaransa linaendelea kuhimiza umoja na mshikamano wa kimataifa katika kukabiliana
na athari za mabadiliko ya tabia nchi sanjari na kuendelea kutekeleza Malengo ya Maendeleo
ya Millenia kwa Mwaka 2015. Huu ni mchakato unaolenga kuboresha maisha ya binadamu
kwa njia ya ushirikiano wa kimataifa bila kugubikwa na utaifa usiokuwa na mguso wala
mashiko. Maskini washirikishwe katika mchakato wa uongozi bora, ili waweze kupanga,
kuamua na kutekeleza masuala yanayohusu mustakabali na hatima ya maisha yao, kwani
hata maskini wanalo jambo la kushirikisha katika ustawi na maendeleo ya binadamu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.