Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, katika
Ibada ya kumsimika Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, Jumapili tarehe
18 Januari 2015, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwapatia heshima ya kulipandisha
hadhi Jimbo la Dodoma kuwa Jimbo kuu, ili kusaidia mchakato wa kupeleka zaidi huduma
za kichungaji kwa waamini, changamoto kwa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dodoma kujenga
na kudumisha misingi ya haki, amani na upendo.
Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania linaungana na Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dodoma kumshukuru Askofu mkuu
Beatus Kinyaiya kwa kukubali uteuzi wa Baba Mtakatifu Francisko wa kuwa Askofu mkuu
wa Jimbo kuu la Dodoma. Hiki ni kielelezo tosha kwamba, Baba Mtakatifu ameridhika
na huduma ya kichungaji iliyokuwa inatolewa na Askofu Beatus Kinyaiya katika Jimbo
Katoliki la Mbulu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linamtaka Askofu mkuu
Kinyaiya kuhakikisha kwamba, anawahudumia kwa ari na moyo mkuu Watu wa Familia ya
Mungu, Jimbo kuu la Dodoma, sanjari na kuendeleza na kuboresha mema yaliyoanzishwa
na Wamissionari wa kwanza Jimbo Dodoma. Aendelee kuchota hekima, ujuzi na maarifa
kutoka kwa watangulizi wake, ili kupambanua matatizo, changamoto na fursa mbali mbali
zilizoko Jimbo kuu la Dodoma, tayari kuzifanyia kazi, kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji
wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Askofu mkuu Kinyaiya
atoe kipaumbele cha kwanza kwa Mungu anapotumia karama na mapaji yake katika kuwafundisha,
kuwaongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu Jimbo kuu la Dodoma; daima akijitahidi
kudumisha amani, upendo na mshikamano wa Familia ya Mungu, Jimbo kuu Dodoma katika
ujumla wake. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanahamasishwa na Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania kutoa ushirikiano wa dhati kwa Askofu mkuu Kinyaiya, ili
aweze kuwatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu kwa kuwajengea imani na matumaini!