2015-01-19 10:38:36

Jimbo kuu la Dodoma!


Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania baada ya kusimikwa rasmi kuliongoza Jimbo kuu la Dodoma, Jumapili tarehe 18 Januari 2015 amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujifunga kibwebwe ili kuombea, kukuza na kudumisha miito mitakatifu, ili Kanisa liweze kuwapata watu mahiri na watakatifu watakaojisadaka kwa ajili ya kuwatangazia watu wa mataifa Injili ya Furaha na Matumaini.

Kwa wale wanaojisikia kwamba, wanaitwa, wanapaswa kufungua mioyo yao kama kijana Samueli ili waweze kuisikia sauti ya Mwenyezi Mungu inayowaita kutoka katika undani wa maisha yao, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa na jamii inayowazunguka. Waamini wanakumbushwa kwamba, miito mitakatifu inachipua na kustawi mahali ambapo waamini wanajitahidi kuwa ni wachamungu, kwa kukuza na kuboresha maisha yao kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma, kielelezo makini cha imani katika matendo.

Askofu mkuu Kinayiya amewataka watanzania kujenga, kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, mshikamano na umoja wa kitaifa, kwani kuna watu katika mataifa mengi duniani wanaoendelea kuteseka kutokana na ukosefu wa misingi ya haki na amani. Umoja na udugu, mafao ya wengi, ustawi na maendeleo ni mambo msingi katika mustakabali wa taifa. Watanzania wajenge ari na moyo wa kupenda kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa na kuachana na tabia ya uvivu, uzururaji na kwamba, kila mwananchi anapaswa kuhakikisha kwamba, anatumia vyema karama na mapaji ambayo amekirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao ya wengi.

Askofu mkuu Kinyaiya, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, wanawafunda na kuwarithisha watoto wao imani, maadili na utu wema, ili kujenga na kudumisha familia, jamii na taifa lenye misingi bora ya maadili na utu wema.

Katika salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, Askofu mkuu Francesco Monteciro Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, ametangaza kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Isack Amani wa Jimbo Katoliki Moshi kuwa ni msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki Mbulu. Na Padre Urbano Sulle atakuwa ni mwakilishi wa Askofu Amani Jimboni Mbulu.

Balozi wa Vatican nchini Tanzania amemtaka Askofu mkuu Kinyaiya kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha Watu wa Mungu Jimbo kuu la Dodoma kwa ari na moyo mkuu, kwa kufuata nyayo za Yesu Kristo, mchungaji wema, aliyejisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti. Amemtaka kukuza utume wa vijana, Jimboni Dodoma kwani hapa kuna bahari ya vijana wengi wanaotoka sehemu mbali mbali za Tanzania ili kujichotea ujuzi na maarifa kutoka kwenye taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu ambavyo viko Dodoma.

Askofu mkuu Padilla, ameitaka Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dodoma kumpatia ushirikiano wa kutosha Askofu mkuu Kinyaiya katika kutekeleza utume na dhamana yake Jimboni humo. Amewashukuru, viongozi mbali mbali waliosaidia mchakato wa maandalizi hadi Jimbo la Dodoma likapewa hadhi ya kuwa ni Jimbo kuu. Ibada ya kusimikwa kwa Askofu mkuu Beatus Kinyaiya imehudhuriwa na Maaskofu Katoliki Tanzania, 27, Askofu mkuu Alex Malasusa, Mkuu wa Kanisa la Kiinjilila Kiluteri Tanzania, Dr. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyemwakilisha Rais Jakaya Kikwete.

Katika hotuba yake kwa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dodoma amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kulipandisha hadhi Jimbo la Dodoma na kuwa Jimbo kuu, kielelezo cha kukua na kukomaa kwa Kanisa; umuhimu wa kujenga, kulinda na kudumisha amani, utulivu, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Rodrick Minja,
Dodoma.







All the contents on this site are copyrighted ©.