Waluteri na Wakatoliki kusherehekea kwa pamoja mageuzi ndani ya Kanisa kunako mwaka
2016
Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani pamoja na Baraza la Kipapa
linalohamasisha Umoja wa Wakristo kunako mwaka 2016, wataadhimisha kwa pamoja Jubilee
ya Miaka 500 tangu mageuzi makubwa yalipofanyika ndani ya Kanisa, maadhimisho ambayo
yatafikia kilele chake hapo mwaka 2017.
Kwa pamoja watashirikishana mafanikio
mbali mbali yaliyokwishafikiwa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya
Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri. Itakumbukwa kwamba, mwaka 2017
Makanisa haya mawili yataadhimisha Jubilee ya miaka 50 ya majadiliano ya kiekumene
kati ya Kanisa la Kiinjili la Kiluteri na Kanisa Katoliki.
Maadhimisho ya Mwaka
2016 yatabainisha maendeleo ya majadiliano ya kiekumene kama yanavyofafanuliwa katika
hati elekezi: kutoka katika kinzani kuelekea umoja; maadhimisho ya pamoja kati ya
Waluteri na Wakatoliki katika mageuzi kwa Mwaka 2017. Hati hii imeandikwa kunako mwaka
2013 kwa ushirikiano kati ya Makanisa haya mawili yanayoangalia kwa umakini mkubwa
mageuzi yaliyofanyika miaka mia tano iliyopita. Hati hii inaonesha mada tete zilizojitokeza
kunako karne ya kumi na sita sanjari na kubainisha maendeleo ya majadiliano ya kiekumene
yaliyofikiwa hadi sasa.
Hati hii inabeba pamoja na mambo mengine, mambo makuu
matano ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene,
ili kutoa ushuhuda wa pamoja wa Makanisa haya mawili. Kuna maelezo ya kiliturujia
yanayoweza kutumiwa na Makanisa haya sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni safari ndefu
ya majadiliano ya kiekumene na kwamba, Jubilee ya miaka 500 ya mageuzi ndani ya Kanisa
ni changamoto ya kiekumene anasema Mchungaji Martin Junge, Katibu mkuu wa Shirikisho
la Makanisa ya Kiluteri Duniani.
Kwa upande wake, Kardinali Kurt Koch, Rais
wa Baraza la Kipapa linalohamasisha Umoja wa Wakristo anasema, waamini wa Makanisa
haya mawili, bado wanaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu na Ukristo;
hivyo, kuna hitaji la kusherehekea kwa pamoja mageuzi yaliyofanywa ndani ya Kanisa.
Hii inatokana na ukweli kwamba, imani ya Kikristo inajikita katika Fumbo la Msalaba,
yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo; mambo msingi yanayobainishwa na Luteri.
Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kusema, kwa mara ya kwanza Waluteri na Wakatoliki
wataweza kuadhimisha mchakato wa kiekumene kwa kuungama kwa pamoja katika hali ya
unyenyekevu imani inayojikita katika Fumbo la Utatu Mtakatifu pamoja na kushikamana
ili kupambana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi
na maendeleo ya sayansi na teknolojia.