Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili mchana tarehe 18 Januari 2015 ameadhimisha Ibada
ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Rizal Park, Jimbo kuu la Manila; ibada ambayo imehudhuriwa
na bahari ya watu kutoka sehemu mbali mbali za Ufilippini. Kwa Ibada ya Fumbo la Ekaristi
Takatifu, Papa amehitimisha hija yake ya kitume nchini Sri Lanka na Ufilippini aliyoianza
tarehe 12 Januari 2015. Ni Ibada ambayo imejikita katika dhamana na utume wa Kanisa
katika Umissionari na kwamba, Familia ya Mungu nchini Ufilippini, inatumwa kuwatangazia
Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu.
Baba Mtakatifu katika mahubiri yake
ameonesha kwa kina na mapana mahusiano yaliyopo kati ya Ufalme wa Mungu na utoto katika
maisha ya kiroho, Habari Njema ya Wokovu; ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi
la dhambi na mauti sanjari na umuhimu wa mwanadamu kujikita katika mchakato wa kutunza
na kudumisha: haki, amani na wajibu. Kila Mkristo anachangamotishwa na Mama Kanisa
kuhakikisha kwamba anajenga na kudumisha Ufalme wa Mungu kama kielelezo cha utambulisho
wao wa Kikristo; kielelezo makini kilichooneshwa na Familia ya Mungu nchini Ufilippini,
ndugu zao walipofikwa na majanga ya tufani ya Yolanda.
Baba Mtakatifu anakumbusha
kwamba, Ufilippini ni nchi ya kwanza ya Kikristo Barani Asia; zawadi kubwa ya Mungu
na baraka kwa watu wake, inayowawajibisha kama sehemu ya wito wao wa Kikristo, ili
kuwa kweli ni mashuhuda na wamissionari mahiri wa imani Barani Asia.
Kwa njia
ya dhambi ya asili, binadamu ameharibu uzuri na kuvunjilia mbali umoja na mshikamano
wa Familia ya binadamu, kwa kujenga na kuanzisha miundo mbinu ambayo ni chanzo kikuu
cha umaskini, ujinga, rushwa na ufisadi. Maandiko Matakatifu yanabainisha kwamba,
tishio kubwa la Mpango wa Mungu kwa mwanadamu daima umekuwa ni uwongo. Shetani ni
baba wa uwongo anayejificha kwa mambo yenye mvuto na mashiko katika mwonekano wake
wa nje kama mambo mapya yanayowatambulisha na wengine katika jamii.
Baba Mtakatifu
anasema, Shetani anawavuta watu kwa mambo yanagusa vionjo vyao vya ndani, raha na
starehe za mpito, kiasi kwamba, watu wanaharibu zawadi na karama mbali mbali ambazo
wamejaliwa na Mwenyezi Mungu; kwa kuchezea maisha na kupoteza fedha kwa kucheza kamari
sanjari na ulevi wa kupindukia, kiasi cha mwanadamu kuharibu maisha yake. Mtu anashindwa
kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mambo msingi katika maisha, katika hali ya unyenyekevu
na hekima kama watoto wadogo, kinyume kabisa na walimwengu! Huu ni ujumbe unaopaswa
kumgusa kila mwamini katika undani wake wa maisha kwa kutambua kwamba, waamini wanaitwa
kuwa ni Familia ya Mungu.
Mtakatifu Nino anawakumbusha waamini kwamba, utambulisho
huu hauna budi kulindwa na kuendelezwa. Mtoto Yesu ambaye ni Mlinzi wa nchi ya Ufilippini
anaendelea kuwahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema, umuhimu wa kulinda
na kutunza familia, Kanisa na Familia ya Mungu ambayo kimsingi ni familia ya binadamu
wote.
Baba Mtakatifu anasema, leo hii kuna haja ya kusimama kidete kulinda
na kutetea familia kwani inakabiliwa na mashambulizi pamoja na programu ambazo kimsingi
ni kinyume kabisa cha Mafundisho ya Kanisa ambayo yanajikita katika wema na utakatifu.
Waamini wanao wajibu na dhamana ya kulinda, kuongoza na kuwatia ari na moyo vijana
pamoja na kuwasaidia kujenga jamii inayojikita katika amani ya maisha ya kiroho na
kitamaduni.
Kanisa linapenda kuona kwamba, kila mtoto ambaye ni zawadi kubwa
kutoka kwa Mwenyezi Mungu anapokelewa, anapendwa na kutunzwa. Kuna haja ya kuwahudumia
vijana, ili kamwe wajanja wachache wasiwapokonye matumaini yaliyomo ndani mwao kwa
kuwatelekeza katika mazingira hatarishi na hatimaye, kuishia barabarani.
Ni
mtoto dhaifu aliyetekeleza mapenzi ya Mungu, kwa kuonesha huruma na haki duniani.
Akaonesha uaminifu mkubwa na kukataa kishawishi cha rushwa; urithi wa dhambi; akashinda
dhambi na mauti kwa nguvu ya Fumbo la Msalaba.
Mara baada ya Ibada ya
Misa takatifu, Askofu mkuu Socrates B. Villegas, Rais wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Ufilippini, amemshukuru Baba Mtakatifu kwa mwanga angavu aliowaletea na kwamba,
mwanga huu, kamwe hautafifia katika maisha yao. Tangu alipowasili nchini Ufilippini,
amewaonjesha watu furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na kwamba, wataendelea kuwa
ni mwanga wa upendo na huruma ya Kristo kwa waja wake, ili kuwasha moto wa Injili
ya Furaha ulimwenguni. Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linamshukuru Baba Mtakatifu
kwa kuwa kweli Mwenyezi Mungu anawapenda na kuwajali!
Naye Kardinali
Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila, amemshukuru Baba Mtakatifu
kwa kuwajali na kuwakumbatia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa
kuendelea kusimama kidete kutetea haki na amani duniani pamoja na utunzaji bora wa
mazingira. Familia ya Mungu nchini Ufilippini inamwahidia Baba Mtakatifu sala, ili
kamwe asitindikiwe na imani, matumaini na mapendo kama Yesu alivyomwambia Mtakatifu
Petro.
Waamini na watu wenye mapenzi mema, wanataka kumsindikiza Baba Mtakatifu
anapokwenda pembezoni mwa jamii, ili kuwasalimia na kuwahudumia wale wanaoishi katika
umaskini na mazingira magumu; wagonjwa. Wanataka kumsindikiza anapowainjilisha wanasiasa,
wachumi, wanasayansi, wanautamaduni na vyombo vya upashanaji habari, ili wote hawa
waweze kuona mwanga wa Kristo ambaye amekuwa ni kiini cha hija yake ya kitume nchini
Ufilippini. Uwanja huu maarufu kwa Serikali na Kanisa; ni mahali ambapo Wamissionari
wapya wanatumwa kueneza mwanga wa Yesu, daima wakiwa wameungana na Khalifa wa Mtakatifu
Petro.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.