2015-01-17 08:23:10

Si bure! Vita huko Mashariki ya Kati!


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki, hivi karibuni ameadhimisha Ibada ya Mkesha kwa ajili ya kuombea amani na utulivu huko Mashariki ya Kati, ibada ambayo imehudhuriwa na waamini wengi wanaotoka katika maeneo haya, ili kumlilia tena Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwakirimia: haki, amani na utulivu baada ya kuteseka sana kwa vita, umaskini, madhulumu na nyanyaso za kidini.

Haya ni mambo ambayo yanaendelea kusababisha mateso makali kwa watu wasiokuwa na hatia, lakini si bure kwani kuna watu ambao wanaendelea kuneemeka kutokana vita na madhulumu yanayofanyika huko Mashariki ya Kati. Kardinali Sandri anawakumbusha waamini kwamba, hata katika mateso na mahangaiko yote haya, Mungu wa agano bado anaendelea kufanya hija pamoja nao, changamoto kwa Wakristo huko Syria na Iraq kubaki imara katika imani na matumaini.

Waamini wamkimbilie na kumlilia tena Mungu kutokana na mapungufu yao ya maisha, ili kuomba huruma, msamaha na upendo wa Mungu! Kwa hakika kuna wafanyabiashara haramu wa silaha na binadamu, wanaendelea kuchuma faida kubwa kutokana na mahangaiko na mateso ya watu wasiokuwa na hatia. Kardinali Sandri, anawaalika wafanyabiashara na wale wote ambao wameweka fedha mbele na kusahau utu na heshima ya binadamu, kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu.

Watu hawa ni sababu na chanzo kikuu cha kuendelea kushamiri kwa matendo ya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia, hali ambayo inaleta kinzani, mateso na mahangaiko na mitafarku kati ya waamini wa dini mbali mbali kama inavyojitokeza huko Nigeria na Mexico. Kardinali Sandri anasema, Kanisa bado lina matumaini kwamba, iko siku, Mwenyezi Mungu ataonesha ukuu na ushindi, kwani ni Bwana wa historia na maisha ya mwanadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.









All the contents on this site are copyrighted ©.