Baba Mtakatifu Francisko, ameianza siku ya Jumamosi, tarehe 17 Januari 2015 kwa kutembelea
Jimbo kuu la Tacloban, ili kusali pamoja na kusalimiana na wahanga wa tufani ya Yolanda
iliyosababisha maafa makubwa kwa wananchi wengi wa Ufilippini. Kutokana na hali ya
hewa kuwa mbaya, mambo kadhaa yaliyokuwa yamepangwa kwenye ratiba ya Baba Mtakatifu
yamefutwa, ili kutoa nafasi kwa Baba Mtakatifu na msafara wake kurejea tena mjini
Manila.
Baba Mtakatifu katika mahubiri yake ameonesha furaha ya kuweza kuadhimisa
Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na wahanga wa maafa ya Yolanda yaliyokuwa na nguvu
za ajabu, lakini yameshindwa kwa upendo wa Mungu, kielelezo makini cha Fumbo la Pasaka,
yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, chemchemi ya maisha na jumuiya mpya, changamoto
ya kujikita katika mambo msingi yanayohudumia utu wa kila binadamu.
Baba Mtakatifu
anawaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kusali kwa ajili ya kuwakumbuka
na kuwaombea wale wote waliofariki dunia, wale ambao bado hajawaonekana na wale walioathirika
zaidi, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwafariji kwa kuwakirimia amani ya ndani. Matukio
magumu kamahaya katika maisha ya mwanadamu yanapaswa kuangaliwa kwa jicho la imani
na matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi, kwani hawa watafarijiwa na Mwenyezi Mungu.
Ni wajibu kwa waamini kumshukuru Mungu aliyewaangalia kwa jicho la huruma
na mapendo walipokuwa katika hali ngumu ya maisha na kwamba, kwa wakati wote huu,
ameweza kuwategemeza licha ya magumu yote haya ndiyo maana wanamshukuru Mungu. Baba
Mtakatifu anawataka waamini kushikamana na Kristo kuhani mkuu kwani ameweza kuchukuana
nao katika udhaifu wao, akajaribiwa sawasawa kama binadamu wengine katika mambo yote
bila kutenda dhambi.
Kwa imani na matumaini haya anasema Baba Mtakatifu ndiyo
maana waamini wanakusanyika tena kumshukuru Mungu baada ya kukumbwa na tufani ya Yolanda,
katika Fumbo la Pasaka, Kristo amebeba ndani mwake, mateso na mahangaiko ya binadamu.
Baba Mtakatifu anashuhudia kwamba, alipoona madhara ya tufani hii, alijisemea moyoni
mwake kwamba, angalipenda kufika katika eneo hili, kuwafariji na kuwaonesha kwamba,
Yesu anawapenda na kamwe hatawaacha pweke, katika shida na mahangaiko yao yote.
Waamini
wayaelekeze macho yao ya imani kwenye Fumbo la Msalaba na hapo Yesu, yuko tayari kuwasindikiza
tena katika hija ya maisha na wakati mwingine katika ukimya! Waamini wamkimbilie Bikira
Maria katika shida na mahangaiko yao, atawaombea na kuwasaidia! Baba Mtakatifu anasema,
kamwe Yesu hawezi kuwaangusha wanapomkimbilia kwa imani na matumaini makuu.
Baba
Mtakatifu Francisko anawashukuru na kuwapongeza wale wote waliojisadaka kwa ajili
ya kuwasaidia na kuwahudumia wahanga wa tufani ya Yolanda. Kundi lote hili ni heshima
kwa Kanisa na taifa katika ujumla wake, ndiyo maana wanamshukuru Mungu kwa kila jambo,
kwani ameendelea kuwa karibu nao katika shida na mahangaiko yao. Baba Mtakatifu anawashukuru
wadau mbali mbali waliowasaidia wananchi wa Ufilippini kutoka sehemu mbali mbali za
dunia, kielelezo makini cha mshikamano wa upendo!
Bado kuna mahitaji makubwa,
kumbe, kuna haja ya kuendelea kuwasaidia wananchi wa Ufilippini ili waweze kusimama
tena na kuendelea na safari yao ya maisha. Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, iwasukume
watu kuguswa na mahangaiko ya jirani zao pamoja na kumwachia Yesu nafasi ili aweze
kuwakomboa kutoka katika ubinafsi na mapungufu yao ya kibinadamu, hasa ubinafsi.
Baba
Mtakatifu anawaalika waamini kumshukuru Mungu kwa miujiza mbali mbali ambayo amewatendea
na anawaweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, msaada wa daima pamoja
na maombezi ya watakatifu kutoka Ufilippini. Wote hawa wasaidia mchakato wa wananchi
wa Ufilippini kujimanua kutoka katika rushwa, ufisadi na ukosefu wa haki mambo yanayochangia
umaskini katika jamii.
Wakati huo huo, Askofu mkuu John F. Du wa Jimbo kuula
Palo, Ufilippini, amemshukuru Baba Mtakatifu kwa kuwatembelea na kuwafariji. Amesimulia
madhara yaliyofanywa na tufani ya Yolanda, lakini kwa imani na matumaini, watu wameweza
kusimama tena na kuendelea na safari ya maisha, huku wakiwa wameshikamana katika umoja
na upendo na kwamba, adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha juu
kabisa cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo. Wanamshukuru
Baba Mtakatifu kwa kuwepo miongoni mwa maskini na waathirika wa tufani ya Yolanda!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.