Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 25 Januari 2015
linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kushiriki katika Novena kama
sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Mtoto ambaye hajazaliwa, inayoadhimishwa kila
mwaka ifikapo tarehe 22 Januari, ili kukumbuka siku ile Mahakama kuu ya Marekani,
kunako mwaka 1973 iliporidhia Sheria ya kutoa mimba! Tayari imekwisha gota miaka 43
tangu tukio hili lilipotokea na kuwashangaza watu wengi nchini Marekani.
Maaskofu
wanasema, kuna sababu nyingi ambazo, waamini wanapaswa kuzifahamu ili kushiriki kikamilifu
katika Novena ya kuombea Injili ya Uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni
mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Ni nafasi
ya kuonesha mshikamano wa upendo na watu wanaoteseka; kusali kwa ajili ya ustawi wa
Kanisa zima, ili kweli liendelee kusimama kidete kulinda, kutetea na kutangaza Injili
ya Uhai na Familia.
Hili ni tukio ambalo linapaswa kukumbukwa, kwani linasaidia
watu kufahamu madhara ya kukumbatia utamaduni wa kifo. Waamini washirikiane na watu
wenye mapenzi mema kwa ajili ya kusali na kutafakari, mambo msingi yatakayosaidia
mchakato wa maboresho katika maisha yao ya kiroho, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda
amini wa Injili ya Uhai miongoni mwa jamii inayowazunguka.
Maaskofu wanawaambia
waamini kwamba, haitoshi tu kusali, bali kuhakikisha kwamba, wanamwilisha sala hii
katika matendo kwa kukataa kukumbatia utamaduni wa kifo, ili kuheshimu kazi ya uumbaji
inayotoa haki msingi kwa kila binadamu kuishi. Siku tisa za kusali kwa ajili ya kuombea
Injili ya uhai ni baraka na neema kubwa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema!
Changamoto ni kusali zaidi!