Boresheni maisha ya maskini na imarisheni haki jamii!
Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 17 Januari 2015 kabla ya kuzungumza na Wakleri,
Watawa, Majandokasisi na wahanga wa tufani ya Yolanda kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu
la Palo, Ufilippini, ametembelea na kufungua Kituo cha Maskini cha Papa Francisko
pamoja na kusalimiana na watoto yatima, wazee na Jumuiya inayowahudumia kwa moyo wa
upendo na huruma.
Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake katika mkutano
huo, amewashukuru wananchi wote wa Ufilippini kutokana na ukarimu wao katika ujenzi
wa maisha mapya baada ya maafa makubwa yaliyosababishwa na tufani ya Yolanda. Hiki
ni kielelezo makini cha uwepo wa Mungu kati ya watu wanaoteseka na kuhangaika katika
maisha pamoja na kuendelea kuwashukuru, wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya kuwahudumia
jirani zao kwa huruma na mapendo, kiasi kwamba, watu wengi wanaliona Kanisa kama alama
ya matumaini mapya.
Hii ni sadaka kubwa itakayozaa matunda kwa vizazi vijavyo.
Baba Mtakatifu Francisko akifanya rejea katika tukio la kubariki na kufungua Kituo
cha Maskini, anasema kwamba, hiki ni kielelezo tosha kabisa cha uwepo wa Kanisa kwa
ajili ya ustawi na maendeleo ya Watu wa Mungu. Hii ni changamoto kwa wanasiasa na
watu wote wenye mapenzi mema, kuwasaidia, kuwahudumia na kuwaheshimu maskini katika
maisha na utu wao kama binadamu.
Sera na mikakati ya kiuchumi isaidie mchakato
wa maboresho ya maisha na mafao ya wengi. Ni mwaliko kwa wanasiasa kuhakikisha kwamba,
wanajenga na kuimarisha haki jamii pamoja na kuwahudumia maskini badala ya kuwatenga
na kuwanyanyasa!
Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, amewashukuru vijana walioshiriki
katika tukio hili pamoja na kuonesha moyo wa upendo na ukarimu ili kuwasaidia wahanga
wa tufani ya Yolanda, changamoto ya kuendeleza mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu
na Utakatifu wa maisha; Hakina Amani nchini Ufilippini.
Wakati huo huo, Familia
ya Mungu nchini Ufilippini imempongeza Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican
anapoadhimisha siku yake ya kuzaliwa. Kutokana na hali ya hewa kubadilika ghafla,
Baba Mtakatifu na ujumbe wake, walilazimika kuondoka mapema huko Tacloban na hivyo
kurejea tena mjini Manila na huo ukawa ni mwisho wa matukio kwa siku ya Jumamosi tarehe
17 Januari 2015.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP. S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.