2015-01-17 11:36:00

Bado kuna shida!


Jopo la Madaktari wasiokuwa na mipaka linasema kwamba, bado kuna watu wengi Kaskazini mwa Nigeria walioshambuliwa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram, wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula unaotishia ongezeko la utapiamlo miongoni mwa watoto, kuna watu ambao wameathirika sana kutokana na mashambulizi haya na kwamba, bado watu hawana uhakika wa usalama wa maisha yao, kumbe wanahitaji huduma ya tiba na chakula!

Wananchi waliopata majeraha makubwa kutokana na mashambuli yaliyofanywa huko Baga hivi karibuni wanaendelea kupata matibabu huko Maiduguri na kwenye eneo la Ziwa Chad. Inasemekana kwamba, kuna bado watu ambao wamejificha msituni kwa kuhofia usalama wa maisha yao.

Jopo la Madtkari wasiokuwa na mipaka hivi karibuni baada ya kuangalia mahitaji msingi, limetoa msaada wa chakula, dawa na vifaa tiba, ili kuokoa maisha ya wahanga wa shambulizi la Baga, ambalo viongozi wengi wa kidini wanasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha mshikamano wao wa dhati ili kupinga vitendo vya kigaidi, vinavyoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Katika kipindi cha miaka mitano Boko Haram imekuwa ni tishio kubwa kwa usalama wa wananchi na mali zao. Kimeendelea kuwatumia watoto wadogo kwa ajili ya mabomu ya kujitoa mhanga, kutekwa makundi makubwa ya watu pamoja na kufanya mashambulizi. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya wakimbizi laki nane hadi millioni moja wanaoishi Kaskazini Mashariki wa Nigeria.







All the contents on this site are copyrighted ©.