2015-01-16 12:11:34

Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi afariki dunia kwa ajali


Askofu Joseph Mukasa Zuza wa Jimbo Katoliki Mzuzu, nchini Malawi ambaye pia alikuwa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, Alhamisi, tarehe 15 Januari 2015 amepata ajali ya gari na kufariki dunia.

Rais Peter Mutharika wa Malawi ametuma salam za rambi rambi kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi kwa kukumbwa na msiba huu mzito. Rais Mutharika anaungana na waamini pamoja na wananchi wote wa Malawi wanaoomboleza msiba wa Askofu Joseph Mukasa Zuza; kiongozi aliyeonesha moyo wa uzalendo na kusimamia mafao ya wengi wakati Malawi ilipokuwa inapitia kipindi kigumu katika historia yake.

Ni kiongozi aliyejisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wake, akawa ni mshirika na mdau mkuu wa ushirikiano na Serikali katika kuwahudumia wananchi wa Malawi. Ni kiongozi aliyekuwa sauti ya kinabii kwa kuwatetea wanyonge na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Atakumbukwa kutokana na huduma yake kwa Familia ya Mungu, Malawi.







All the contents on this site are copyrighted ©.