Pambaneni na changamoto za kiimani na kimaadili kwa ujasiri!
Marais wa Tume za Mafundisho Tanzu ya Kanisa waliokuwa wanafanya mkutano wao huko
Esztergom, Hungaria, wamehitimisha mkutano wao uliokuwa unasimamiwa na Kardinali Gerhard
L. Muller, Rais wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, aliyesoma ujumbe
wa Baba Mtakatifu Francisko na baadaye kufafanua kwa kina na mapana umuhimu wa Mabaraza
ya Maaskofu katika urika wao wanapofundisha, ongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu.
Kardinali Muller amewakumbusha Marais hao umuhimu wa kujenga na kudumisha
umoja sanjari na kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa kuwarithisha
vijana imani na maadili mema kadiri ya mafundisho ya Kanisa. Ulikuwa ni wakati kwa
wajumbe kupembua kwa kina na mapana changamoto wanazokabiliana nazo katika mikakati
ya shughuli za kichungaji na kwamba, Kanisa halina budi kusimama kidete kulinda na
kudumisha Injili ya Uhai.
Kardinali Muller amewakumbusha Maaskofu kwamba, wao
ni walimu wa imani, inayopaswa kufundishwa na kurithishwa kwa waamini huku wakiwa
wameungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Watambue kwamba, wokovu ni zawadi ambayo
inatolewa na Kristo kwa kila mtu, kumbe ni jukumu la Kanisa Barani Ulaya kuendelea
kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu. Maaskofu wamejadili pamoja na
mambo mengine, nadharia, uelewa wa mafundisho ya Kanisa kuhusu binadamu; uhuru wa
kidini pamoja na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika Uinjilishaji Mpya Barani
Ulaya.
Wajumbe wamepembua kwa kina na mapana kuhusu umuhimu wa Sakramenti ya
Upatanisho; jukumu na dhamana ya Tume ya Maaskofu kuhusu mafundisho tanzu ya Kanisa;
mada ambazo zimejadiliwa katika hali ya utulivu na maelewano makubwa miongoni mwa
wajumbe. Jioni ilikuwa ni nafasi ya kufahamiana na kubadilishana mawazo na mang'amuzi
kuhusu mikakati ya shughuli za kichungaji Barani Ulaya. Mkutano huu imekuwa ni fursa
ya kuimarisha mshikamano na umoja kati ya Tume za Maaskofu Katoliki Barani Ulaya na
Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, ili kukabiliana kikamilifu na changamoto
za mafundisho tanzu ya Kanisa Barani Ulaya kwa ujasiri mkubwa.