2015-01-16 11:11:20

Msiamshe hasira za watu kwa kukufuru dini!


Baba Mtakatifu Francisko anasema, maskini ndiyo ujumbe wake mkuu nchini Ufilippini pamoja na kuwaimaarisha ndugu zake waliokumbwa na majanga asilia, ili waweze kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa. Baba Mtakatifu anasema, uhuru wa kujieleza ni haki msingi na kwamba, kuna haja ya waandishi wa habari kutofanya kufuru kwa dini za watu wengine, na kwamba, anajiandaa kutoa waraka wake wa kichungaji kuhusu mazingira! Haya ni kati ya mambo msingi yaliyozungumzwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa waandishi wa habari wakati alipokuwa njiani kuelekea nchini Ufilippini, Siku ya Alhamisi tarehe 15 Januari 2015.

Baba Mtakatifu anasema, si haki kufanya mauaji kwa kisingizio cha kidini na kwamba, mtu anatenda kosa kufanya kufuru dhidi ya dini ya mwingine. Kumbe, kuna haja ya kusema na kuandika mambo msingi yanayosaidia kukuza na kudumisha mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu pamoja na dini ikipewa nafasi yake katika maisha ya kijamii.

Baba Mtakatifu anapoangalia majanga mbali mbali yanayoendelea kujitokeza katika uso wa nchi anasema kwamba, ni matokeo ya matumizi mabaya ya rasilimali ya dunia ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu. Waraka wake wa kichungaji unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mwezi Juni au mwanzoni mwa Mwezi Julai 2015. Muswada wa kwanza umekwishaandikwa na Baraza la Kipapa la haki na amani; muswada wa pili akaupitia mwenyewe na sasa anataka kuwapatia wanataalimungu ili waweze kuuangalia, ili uweze kuwa kweli ni mchango mkubwa wa Kanisa katika kukabiliana na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi katika mkutano wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika mjini Paris mwaka 2015.

Baba Mtakatifu anasema, amesikitishwa na matokeo ya mkutano wa Jumuiya ya Kimataifa kuhusu mazingira uliokuwa unafanyika nchini PerĂ¹ kwa wajumbe wake kukosa ujasiri wa kufanya maamuzi machungu.

Baba Mtakatifu anasema, katika mchakato wa Uinjilishaji mpya anapenda kutoa kipaumbele cha kwanza kwa wenyeheri waliojisadaka kwa ajili ya kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu. Hivi ndivyo alivyofanya kwa kumtangaza Mwenyeheri Angela wa Foligno, Pietro Favre na Padre Joseph Vaz. Anatarajiwa kumtangaza Junipero Serra kuwa Mtakatifu wakati wa hija yake ya kichungaji nchini Marekani mwezi Septemba 2015.

Baba Mtakatifu amesikitishwa na kukemea vikali vitendo vya kuwatumia watoto wadogo katika mashambulizi ya mabomu ya kujitoa mhanga kama inavyojitokeza huko nchini Nigeria kwamba, matukio haya yanaonesha matatizo makubwa katika maisha ya mwanadamu kwa kuamua kuuwa ili kuuwawa badala ya kutoa kilicho chema. Watu wanapaswa kujisadaka kwa ajili ya ujenzi wa mambo mema na wala si kwa ajili ya mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Mabomu ya kujitoa mhanga wanayovishwa watoto wadogo ni namna nyingine tena ya utumwa mamboleo.

Kuhusu magaidi wanaotishia kuishambulia Vatican, Baba Mtakatifu anasema, hofu yake kubwa ni watu wanaofurika kila siku mjini Vatican ili kusali na kukutana naye, lakini kwake binafsi hana kitu cha kumwogofya sana anaweza kukabiliana na vitisho hivi kwa kujivika fadhila ya unyenyekevu. Kuna waamini wa dini mbali mbali wanaendelea kulivalia njuga tatizo la ugaidi wa kimataifa, lakini bado linafanyiwa kazi.

Baba Mtakatifu anasema, aliomba kutembelea na kusalimiana na waamini wa dini ya Kibudha kwenye Hekalu lao, ili kuonesha heshima na upendo waliomkirimia kwa kufika Uwanja wa ndege kumpokea wakati alipokwenda nchini Sri Lanka, changamoto ya kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali kama sehemu ya ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana na kuthaminiana. Katika Madhabu ya Madhu, Baba Mtakatifu anasema, ameshuhudia waamini wa dini ya Kibudha wakiwepo ambayo ni kwa hakika ni dalili njema.

Mchakato wa upatanisho, haki na amani katika ukweli ni uwazi ni mambo ambayo Baba Mtakatifu anaendelea kuyapatia kipaumbele cha kwanza, kama alivyofanya nchini Sri Lanka na Argentina. Amempongeza Rais wa Sri Lanka anayetaka kuendeleza mchakato wa amani na upatanisho kwa ajili ya mafao ya wengi nchini mwake. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha mazungumzo na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kutoka Colombo kuelekea Manila kwa kulitakia Shirika la Habari la ANSA heri na fanaka linapoadhimisha Miaka 70 ya huduma iliyotukuka katika tasnia ya habari duniani. Mazungumzo haya yamedumu kwa takribani dakika 45.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.