2015-01-16 11:20:34

Kiongozi!


Katika somo la Kwanza – tunasikia habari juu ya Samweli na sauti ya Mungu na mwongozo wa Eli. Samweli alikulia katika mazingira ya Mungu chini ya maongozi ya mama yake, halafu chini ya uongozi wa kuhani Eli, katika mazingira ya uongozi wa dini na kumjua Mungu. Lakini sauti ya Mungu iliposikika kwake binafsi hakuielewa. Ni kwa njia ya Eli aliweza kutambua mwito huo wa Mungu. Kwa nini Mungu afanye hivyo?

Mungu hufanya kazi kwa namna yake, akitumia watu wake au vyombo mbalimbali kama kanisa. Neno la Mungu katika Ebr. 5:1, litusaidie katika kuelewa hili - maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi.

Katika somo la II – Mtume Paulo anaweka bayana hali inayomtambulisa mkirsto – na akitaja wazi usafi. Na mwili ni kwa ajili ya Bwana na si vinginevyo. Hivyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu. Mwili si chombo tu.

Katika Injili – Andrea na Yohane walimfuata Yohane Mbatizaji huku wakimngojea masiha. Kwa muda mrefu walisali na kufunga – lakini walipokutana naye hawakumtambua. Tena alihitajika Yohane mbatizaji kuwatambulisha. Hitaji la kuhani kama Eli au nabii kama Yohani bado liko pale pale ili kutuonesha Mungu, Yesu Kristo.

Hapa tunamwona Yohane akiwa bado yuko kwenye kingo za mto Yordani na Yesu anapita – anamtambua na anawaambia wanafunzi wake – tazama mwanakondoo wa Mungu, nao mara wakamwacha kabisa Yohane na kumfuata Yesu. Naye Yesu hakusita kuwauliza alipowaona wanamfuata –mnatafuta nini? Wao wakajibu – mwalimu unakaa wapi? Yesu akajibu – njoo muone. Wao – wakaenda, wakaona, wakabaki naye. Tukio muhimu sana kwao, wanakumbuka hata muda – karibia saa 10 jioni.

Hitaji kama hili bado liko wazi hata leo. Hitaji la kiongozi. Lakini kiongozi bora kama Yohani Mbatizaji na si bora kiongozi. Watu wengi hudhani kufahamu au kujua yote na hivyo kutokuhitaji ushauri wala mawaidhwa yahusuyo maisha na mambo ya Mungu. Tusisahau kuwa mganga hajigangi. Na si kila mshauri tu afaa. Tunahitaji yeye mwenye roho wa Mungu.

Angalia habari juu ya towashi mkushi aliyekuwa akisoma sehemu ya maandiko matakatifu – Mdo. 8, 30-31 basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, je yamekuelea haya unayosoma? Akasema, nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye. Ili kuelewa maandiko alihitaji muelekezi – ambaye kwake ni mtume Filipo.

Pia katika 2Pt. 1:20-21; tunasoma neno hili - mkijua neno hili kwanza; ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu, bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.

Ndugu zangu, leo tunatafakarishwa tena haja ya kuwa watumishi waaminifu wa Mungu. Na anayeishi kadiri ya mapenzi yake Mungu atakuwa kiongozi hodari. Kina kuhani Eli, kina nabii Yohane Mbatizaji wanahitajika sana leo na katika maisha na mazingira yetu. Kila mmoja wetu ajisikie leo baada ya kusikia neno hili kuwa na deni. Deni la ushuhuda ili wengine watufuate, deni la kiongozi bora, deni la watafsiri hodari wa Neno la Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.