Askofu mkuu mteule Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania anatarajiwa kusimikwa
rasmi hapo tarehe 18 Januari 2015, kadiri ya taarifa iliyotolewa na Askofu Bernadine
Mfumbusa, Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki Dodoma. Askofu mkuu mteula anatarajiwa
kuwasili katika Makao Makuu ya Jimbo Katoliki Kondoa tarehe 16 Januari 2015 na kupumzika
hapo akiwa anatokea Jimbo Katoliki la Mbulu.
Waamini wa Jimbo kuu Katoliki
la Dodoma watampokea Askofu mkuu wa kwanza wa Dodoma hapo tarehe 17 Januari 2015 mpakani
kwa Jimbo kuu la Dodoma na Kondoa. Atakapowasili Jimboni Dodoma atakabidhiwa ufunguo
wa Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba na hapo masifu ya Jioni yataanza.
Itakumbukwa
kwamba, Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alilipandisha hadhi Jimbo Katoliki
la Dodoma na hivyo kuwa Jimbo kuu la Dodoma linaloyajumuisha Majimbo ya Singida na
Kondoa, Tanzania na kumteua Askofu Beatus Kinyaiya kuwa Askofu mkuu wa kwanza wa Jimbo
kuu la Dodoma, ili kusogeza zaidi huduma za kichungaji kwa Familia ya Mungu, Kanda
ya kati nchini Tanzania.
Askofu mkuu mteule Beatus Kinyaiya alizaliwa kunako
tarehe 9 Mei 1957, Shimbwe, Jimbo Katoliki la Moshi. Baada ya masomo yake ya shule
ya msingi, alibahatika kuchaguliwa kuendelea na masomo ya Sekondari Seminari ndogo
ya Maua iliyoko Jimbo Katoliki la Moshi na baadaye akaendelea pia na masomo yake ya
kidato cha tano na sita kwenye Seminari ya Itaga, iliyoko Jimbo kuu la Tabora. Baada
ya masomo na majiundo yake ya maisha ya kitawa katika Shirika la Ndugu Wadogo, maarufu
kama Wakapuchini, aliweka nadhiri zake za daima kunako tarehe 25 Juni 1988.
Askofu
mkuu mteule Beatus Kinyaiya alisoma Falsafa Seminarini kuu ya Kibosho iliyoko Jimbo
Katoliki la Moshi na kuhitimu masomo yake ya Kitaalimungu kwenye Seminari ya Mtakatifu
Charles Lwanga, maarufu kama Segerea, iliyoko Jimbo kuu la Dar es Salaam. Baadaye
alitumwa na Shirika kwenda kuendelea na masomo ya juu kwa kujikita zaidi katika masomo
ya: historia, jiografia na falsafa huko London, Uingereza.
Baada ya kuhitimu
masomo yake nchini Uingereza, alirejea tena nchini Tanzania na hapo akapangiwa kuwa
ni Gombera Msaidizi na Mwalimu katika Seminari Ndogo ya Maua, iliyoko Jimbo Katoliki
la Moshi, utume ambao aliufanya kati ya mwaka 1989 hadi mwaka 1992. Kuanzia mwaka
1996 hadi mwaka 1999 alikuwa ni Gombera wa Seminari ndogo ya Maua. Aliwahi kuwa ni
mkuu wa Shirika la Wakapuchini nchini Tanzania na Mwenyekiti wa Wakuu wa Mashirika
ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Tanzania kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2005.
Baada
ya kujiendeleza zaidi katika masomo ya maisha ya kiroho kutoka Chuo kikuu cha Kipapa
cha Antonianum, kilichoko mjini Roma, aliteuliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto
XVI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu tarehe 22 Aprili 2006 na kuwekwa wakfu
kuwa Askofu hapo tarehe 2 Julai 2006. Kwa ufupi, hili ndilo “Jembe jipya” la Jimbo
kuu la Dodoma, Tanzania.
Tukio hili linatarajiwa kuhudhuriwa na umati mkubwa
wa waamini kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Dodoma.
Na Padre Richard A.
Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.