Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa jioni tarehe 16 Januari 2015 amekutana na kuzungumza
na Familia mbali mbali kutoka Ufilippini, kwa kuwashukuru kwa ushuhuda wa imani inayomwilishwa
katika maisha ya kila siku. Katika tafakari yake, Baba Mtakatifu amekazia mambo makuu
matatu; kupumzika katika Kristo; kusimama na Yesu pamoja na Bikira Maria pamoja na
kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii!
Baba Mtakatifu anasema mapumziko katika
Kristo ni jambo muhimu sana kwa ajili ya maisha ya kiroho na kimwili, changamoto kwa
Wakristo kujenga familia na Yesu kama alivyofanya Mtakatifu Yosefu; mchakato unaopaswa
kujikita kwanza kabisa katika mioyo, parokia na jumuiya zao. Kupumzika katika Kristo
kunamaanisha kujenga mahusiano mema na Kristo kwa njia ya Sala, inayokuwa ni nguvu
na kichocheo cha kuendelea na kazi na kamwe Wakristo wasiwe ni wavivu katika sala,
vinginevyo watashindwa kutambua uwepo wa Mungu kati yao. Sala ina nafasi ya pekee
katika maisha ya kifamilia.
Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, familia ni shule
ya kwanza ya sala, fursa ya kukua na kufanya hija ya pamoja kama watu wa imani na
kujiangalia kama sehemu ya Familia kubwa ya Mungu, yaani Kanisa. Ni shule inayowasaidia
watu kujisadaka kwa ajili ya wengine, kwa kuondokana na ubinafsi na kushirikishana
zawadi ya maisha na watu wengine. Hii ndiyo maana Familia ni muhimu sana katika maisha
na utume wa Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko anazitaka familia za Kikristo
kusimama pamoja na Yesu na Maria kama alivyofanya Mtakatifu Yosefu kwa kusoma alama
za nyakati, baada ya kuamka kutoka usingizini, ili kutekeleza wajibu wake. Imani haimwondoi
mwamini ulimwenguni, lakini inamsaidia kuingia zaidi katika ulimwengu kwa kutenda
na kusaidia mchakato wa kuandaa ulimwengu kwa ajili ya ujio wa Mungu katika utimilifu
wa nyakati. Leo hii anasema Baba Mtakatifu, familia zinakabiliwa na matatizo, changamoto
na kinzani nyingi.
Ufilippini ambako wamekabiliana na majanga asilia yaliyosababishwa
na tufani pamoja na hali ngumu ya uchumi; ni kati ya mambo ambayo yamechangia kwa
kiasi kikubwa kwa watu wengi wa Ufilippini kuhama kutoka katika nchi yao kwa kutengana
na familia zao; ukosefu wa fursa za ajira na ukata katika familia nyingi ni matatizo
ambayo yanaendelea kujitokeza katika maisha na utume wa familia nchini Ufilippini.
Kuna kundi kubwa la familia linaloishi katika umaskini wa kutupwa, wengine wamemezwa
na malimwengu kiasi hata cha kuharibu tunu msingi za maisha ya maadili, utu wema na
Kikristo katika familia.
Baba Mtakatifu anazialika familia za Kikristo kujifunga
kibwebwe ili kupambana na mawazo mepesi mepesi; utamaduni wa "kuganga tumbo kwa siku
moja", tatizo la kutema zawadi ya maisha kwa kukumbatia utamaduni wa kifo unaopigiwa
"debe" na baadhi ya taasisi mintarafu maisha ya ndoa. Mtakatifu Yohane Paulo II katika
Waraka wake wa kichungaji kuhusu wajibu wa Familia za Kikristo anabainisha kwamba,
ubinadamu kwa siku za usoni unarithishwa kwa njia ya familia, changamoto kwa watu
kusimama kidete kusaidia familia ili kujenga jamii.
Baba Mtakatifu Francisko
kwa namna ya pekee anawataka wakristo nchini Ufilippini kuimaarisha familia kwani
hii ni rasilimali kwa ajili ya jamii nzima na kwamba, wito wa familia za Kikristo
unarutubishwa kwa njia ya Sala, Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya
huruma, changamoto kwa Wakristo kuhakikisha kwamba, wanatunza na kulinda familia kama
Madhabahu ya Injili ya Uhai, kwa kuheshimu zawadi ya maisha, tangu pale mtoto anapotungwa
mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa
Mungu.
Mwishoni, Baba Mtakatifu anazitaka familia za Kikristo kuwa kweli ni
Sauti ya Kinabii kati ya watu wanaowazunguka kama alivyofanya Mtakatifu Yosefu, kwa
kuwa wasikivu na makini kwa wito wa Mungu kwa Bikira Maria na Mtoto Yesu. Kwa njia
hii Mtakatifu Yosefu aliweza kuingia katika Mpango wa Mungu na kuwa kweli ni baraka
kwa binadamu wote.
Kwa njia ya Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, Familia za
Wafilippini hazina budi kuwa ni mfano bora wa vijana kukua katika neema, huku wakiwa
makini katika tunu msingi za maisha, ili kweli waweze kuwa baraka kwa jamii nzima.
Katika mantiki hii, upendo kwa Mungu unakuwa ni nguvu ya jamii na hivyo kusaidia katika
mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu duniani, ili kutekeleza dhamana waliojitwalia
kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo.
Baba Mtakatifu anaunganisha tabia ya kimissionari
katika familia na maadhimisho ya Mwaka wa Maskini; hivyo anawaalika wananchi wa Ufilippini
katika ujumla wao kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wahitaji zaidi; watu wanaokosa
msingi bora wa kifamilia, wazee na watoto yatima; ambao mara nyingi wanasahaulika
hata na majirani zao wa karibu. Watu hawa wahudumiwe si tu katika mahitaji yao ya
kimwili, bali iwe pia ni zawadi ya kukutana na Kristo sanjari na Kanisa kama Jumuiya.
Naye Askofu Gabriel Reyes, Mwenyekiti wa Tume ya Familia, Baraza ya Maaskofu
Katoliki Ufilippini anasema, kwao familia ni kiota cha furaha; mahali panapobubujika
joto, lakini pia kuna baadhi yao wachenganyikiwa na kutembea katika giza; baadhi yao
wamechoka na kutumbukia katika upweke hasi; kumbe maneno ya Baba Mtakatifu Francisko
yamewaimarisha na kuwapatia nguvu ya kusonga mbele kwa imani na matumaini.
Familia
mbali mbali nchini Ufilippini zimeshuhudia kwamba, zinadhamana ya kuendeleza utume
wa familia duniani, kwa kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa kwa kuwajali
na kuwahudumia maskini, huku wakitambua kwamba, wao ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji
mpya.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.