2015-01-16 11:29:15

Bahari ya Mediterania ni kaburi la wahamiaji wengi!


Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, inayoadhimishwa na Mama Kanisa hapo tarehe 18 Januari 2015, linaiomba Serikali ya Hispania kuwasikiliza kwa makini wakimbizi kabla ya kuchukua maamuzi machungu ya kuwafukuza nchini humo.

Ni wajibu wa Serikali kuangalia shida za wakimbizi na wahamiaji hawa ikiwa kama ni watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, au ni watu ambao ni wahanga wa vita na kinzani za kisiasa au kundi ambalo limetumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo kutokana na uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka.

Baada ya kuangalia sababu zote hizi, hapo Serikali inawajibu wa kutekeleza sheria za kimataifa mintarafu wahamiaji na wakimbizi, vinginevyo ni kutowatendea haki watu hawa ambao wanakumbana na majaribu makubwa katika maisha yao. Kwa kuwasikiliza kwa makini anasema Askofu Ciriaco Benavente wa Jimbo Katoliki Albacete, Hispania, Serikali inaweza kufanya maamuzi ya haki na usawa.

Inasikitisha kusema kwamba, Bahari ya Mediterania kwa sasa imekuwa ni kaburi kuu la wahamiaji na wakimbizi wanaokimbia nchi zao kutokana na sababu mbali mbali, kwa matumaini ya kupata maisha bora, lakini wanajikuta wakimezwa na kufukiwa kwenye Bahari ya Mediterania na huo ndio unakuwa ni mwisho wa ndoto ya maisha bora zaidi. Hispania na Italia kwa sasa ni kati ya nchi ambazo zinapokea idadi kubwa ya wahamiaji na wakimbizi na taarifa zinazonesha kwamba, zaidi ya watu 3, 000 wamekufa maji huko Hispania na kati yao kuna watoto 15.

Takwimu zinaonesha kwamba, Hispania inatoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji millioni 5. Askofu Benavente amewakumbusha wananchi wa Hispania ambao wamesahau kwamba, hata Jamii kubwa ya Hispania ni watoto wa wahamiaji na wakimbizi, kumbe wanapaswa kuguswa na mahangaiko ya watu hawa badala ya kuwatelekeza katika shida na mahangaiko yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.