2015-01-15 09:10:39

Ujumbe kwa Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani kwa Mwaka 2015


Kanisa bila mipaka kwani ni mama wa wote ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani, inayoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 18 Januari 2015. Mama Kanisa anahamasishwa kuhakikisha kwamba, anafungua mikono yake ili kuwakaribisha watu wote bila ubaguzi wala kikomo. RealAudioMP3

Baba Mtakatifu anasema, Yesu Kristo ndiye Mwinjilishaji mkuu, aliyeonesha upendeleo mkubwa kwa watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, anwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwahudumia wale wanaosumbuka na kuteseka, kwa kutambua ndani mwake mateso ya watu wanaotumbukizwa katika mifumo mipya ya umaskini na utumwa, kwa njia ya matendo ya huruma.

Kanisa katika utume wake, linatambua kwamba ni hujaji hapa ulimwenguni na Mama wa wote, hivyo linahamasishwa kumpenda na kumwabudu Yesu Kristo anayejionesha kati ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kati yao ni: wahamiaji na wakimbizi, wanaotafuta nafuu ya maisha kwa kukimbia magumu wanayokabiliana nayo. Ndiyo maana anasema Baba Mtakatifu Francisko, kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi kwa mwaka huu ni “Kanisa bila mipaka, Mama wa wote”.

Kanisa linafungua mikono yake na kuwakaribisha watu wote bila ubaguzi au kikomo, ili kuwatangazia kwamba, Mungu ni upendo. Yesu Kristo mara baada ya kufufuka kwake aliwakabidhi wafuasi wake utume wa kushuhudia na kutangaza Injili ya Furaha na Huruma. Siku ile ya Pentekoste, mitume walijitokeza hadharani, wakiwa wameimarishwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu wakashinda woga na mashaka yaliyokuwa yamejikita mioyoni mwao na wote waliosikia Habari Njema ikitangazwa masikioni mwao, wakaelewa ujumbe huo katika lugha zao wenyewe.

Tangu mwanzo, Kanisa limekuwa ni Mama ambaye moyo wake uko wazi na bila mipaka. Utume huu umeendelezwa kwa takribani miaka elfu mbili sasa. Tangu mwanzo, Wamissionari walitangaza na kushuhudia Umama wa Kanisa, dhana ambayo iliendelezwa na Mababa wa Kanisa na kufanyiwa kazi kwa umakini zaidi na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, walipotamka kuwa Kanisa ni mama, Ecclesia Mater, ili kufafanua asili ya Kanisa linalowakumbatia wote moyoni mwake kwa njia ya upendo.

Kanisa mama wa wote pasi na mipaka, limeenea sehemu mbali mbali za dunia, ili kuendeleza utamaduni wa ukarimu na mshikamano kwa kutambua thamani ya kila binadamu. Kanisa linapoishi kikamilifu dhana hii ya umama, Jumuiya za Kikristo zinarutubishwa, zinaelekeza na kuonesha njia, zinawasindikiza watu kwa uvumilivu na kuwakumbatia kwa njia ya sala na matendo ya huruma.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, yote haya yanapata maana mpya kutokana na ukweli kwamba, kuna wimbi kubwa la wahamiaji linalokimbia nchi zao, wakiwa wamebeba masanduku ya woga na matumaini wakiwa tayari kuanza safari ya matumaini, lakini inayosheheni hatari, ili kutafuta maisha bora zaidi. Kwa bahati mbaya, wahamiaji hawa wanakumbana na hali ya kinzani hata katika Jumuiya za Kikanisa bila hata ya kujitaabisha kufahamu historia ya madhulumu na hali ya kukatisha tama.

Ni watu wanaoangaliwa kwa “jicho la kengeza”, wanaotiliwa mashaka kiasi hata cha kuweka kando Amri ya Maandiko Matakatifu inayowataka waamini kuwakaribisha kwa heshima na mshikamano wageni wenye shida. Kutoka katika undani wa dhamiri nyofu, waamini wanahimizwa kugusa mateso na mahangaiko ya wahamiaji ili kuwaonjesha amri ya upendo ambayo Yesu amewaachia wafuasi wake. Wageni hawa ni wale wanaoteseka, wahanga wa madhulumu na unyonyaji; wote hawa waonjeshwe ukarimu wa Kristo kama njia ya kuendelea kuganga madonda ya Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ujasiri unaoibuliwa kutoka katika imani, mapendo na matumaini inawawezesha waamini kupunguza umbali uliopo kati yao na umaskini wa watu. Yesu anasubiri kutambuliwa kati ya wahamiaji na wakimbizi; kati ya wale wanaoteseka na kunyanyasika ugenini na kwa njia yao, Yesu anawahamasisha wafuasi wake kuwashirikisha rasilimali pamoja na kuwamegea kidogo, utajiri ambao Mwenyezi Mungu amewakirimia katika maisha yao, ili uweze kutumika kwa ajili ya mafao ya wengi kama anavyokazia Mwenyeheri Papa Paulo VI.

Jamii mamboleo inajionesha katika tamaduni mbali mbali. Ndiyo maana Mama Kanisa anawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika mshikamano, umoja na uinjilishaji. Makundi ya wahamiaji ni changamoto kwa Kanisa kuhakikisha kwamba, linakuza na kuimarisha tunu msingi zitakazodumisha amani na utulivu kati ya watu na tamaduni. Watu wenye tamaduni na asili tofauti wanapaswa kuheshimiana, kwa kuvunjilia mbali tabia ya watu kujikita katika woga usiokuwa na mashiko na kutaka kujilinda wenyewe kwa kutowajali wakimbizi na wahamiaji. Mama Kanisa anahamasisha utamaduni wa watu kukutana, ili kujenga dunia iliyo bora zaidi inayojikita katika haki na udugu.

Makundi makubwa ya wahamiaji yanayoendelea kujitokeza katika uso wa dunia anasema Baba Mtakatifu, yanahitaji ushirikiano wa dhati kati ya Serikali na Mashirika ya kimataifa, ili kudhibiti na kuratibu mwenendo wa wahamiaji na wakimbizi kwa ufanisi zaidi mintarafu masuala ya: kijamii, kiuchumi, kisiasa, kitamaduni na kidini sanjari na matatizo na changamoto zote zinazoweza kujitokeza katika masuala kama haya kitaifa na katika ngazi ya Kimataifa.

Katika ngazi ya Kimataifa kumekuwepo na mijadala inayogusia wajibu, mbinu na sheria zinazoweza kutumika kwa ajili ya kudhibiti wimbi la wahamiaji na wakimbizi, huduma inayotolewa na wadau katika ngazi mbali mbali, lakini utekelezaji wa sera na mikakati hii yamebaki kuwa ni maneno matupu kuliko vitendo, changamoto ya kutekeleza sera hizi kwa njia ya ushirikiano wa kimataifa, kwa kuheshimu utu na mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza. Hali hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kupambana na biashara haramu ya binadamu ambayo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu, inayowapoka watu haki zao msingi kwa kuwatumbukiza katika mateso, dhuluma na utumwa.

Baba Mtakatifu anasema, ushirikiano wa pamoja unahitaji kujikita katika umoja, kwa kubainisha mbinu mkakati shirikishi, ukweli na uwazi, kwani hakuna nchi ambayo inaweza kujigamba kwamba inaweza kukabiliana na tatizo la wahamiaji na wakimbizi kwa jeuri yake yenyewe. Uhamiaji wa utandwazi unaweza kudhibitiwa kwa kujikita katika utandawazi wa upendo na ushirikiano ili kuboresha hali ya maisha ya wakimbizi na wahamiaji duniani, sanjari na kuhakikisha kwamba, mambo yote yanayosababisha watu kuzikimbia nchi zao yanadhibitiwa kikamilifu. Sababu kubwa ni vita na njaa; mambo yanayowalazimisha watu kuzikimbia nchi zao.

Baba Mtakatifu anasema, mshikamano na wahamiaji pamoja na wakimbizi hauna budi kusindikizwa na ujasiri pamoja na kipaji cha ugunduzi, kinachoweza kutekelezwa katika ngazi ya kimataifa kwa kudumisha haki na usawa katika masuala ya fedha na uchumi na kuendelea kujikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha amani, kichocheo kikuu cha maendeleo endelevu ya watu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaambia wahamiaji na wakimbizi kwamba, wao wanayo nafasi ya pekee katika moyo wa Kanisa na kwamba, wanalisaidia Kanisa kuonesha umama wake kwa familia ya binadamu. Anawataka kukuza na kudumisha imani na matumaini, kwa kutambua ujasiri wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu iliyolazimika kukimbilia Misri, ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu. Kwa hakika Mwenyezi Mungu hataweza kuwaacha katika shida na mahangaiko yao kama alivyofanya kwa Familia Takatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.