2015-01-15 08:45:15

Papa Francisko awasha cheche za matumaini nchini Sri Lanka!


Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 14 Januari 2015 ametembelea Hekalu la Wabudha, akakutana na Baraza la Maaskofu Katoliki Sri Lanka pamoja na kuzungumza na Rais wa zamani wa Sri Lanka aliyekuwa ameambatana na familia yake!

Itakumbukwa kwamba, Rais mstaafu Mahinda Rajapaksa ndiye aliyekuwa amemwalika rasmi Baba Mtakatifu Francisko kutembelea nchini Sri Lanka, lakini siku chache tu kabla ya kuwasili kwa Baba Mtakatifu nchini humo akashindwa kwenye uchaguzi mkuu.

Baba Mtakatifu amemshukuru kwa maandalizi mazuri yaliyofanikisha hija yake ya kitume nchini Sri Lanka, lakini kwa namna ya pekee, amani, utulivu, umoja na mshikamano wa kitaifa uliojionesha mara baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu kutangazwa rasmi. Tukio hili limeonesha ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia nchini Sri Lanka.

Padre Lombardi anasema, Baba Mtakatifu ametembelea Hekalu la Kibudha na kusalimiana na viongozi wake wakuu, akapewa maelezo ya kina kuhusiana na nyumba hii ya sala, inayofunguliwa mara moja kwa mwaka. Wakati huu, Hekalu hili lilifunguliwa kwa heshima ya Baba Mtakatifu Francisko, kama kielelezo cha heshima, upendo na urafiki katika mchakato wa majadiliano ya kidini unaofumbatwa katika utamaduni wa watu kukutana.

Baba Mtakatifu aliweza kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Sri Lanka kwenye Makao makuu ya Jimbo kuu la Colombo. Baba Mtakatifu amebadilishana mawazo na Maaskofu katika hali ya urafiki na upendo mkuu. Kutokana na matatizo ya usafiri kutoka kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu Madhu, Maaskofu walichelewa kidogo, lakini Baba Mtakatifu aliwasubiri na baadaye akazungumza nao kwa kukazia umuhimu wa Padre Joseph Vaz kutangaza kuwa Mtakatifu na kwamba, atasaidia kukoleza mchakato wa Uinjilishaji Mpya nchini Sri Lanka, unaojikita katika majadiliano ya kidini, haki, amani na upatanisho.

Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru kwa namna ya pekee, wananchi wa Sri Lanka kwa kumpatia hundi ya dolla za kimarekani sabini elfu, ili kuwasaidia maskini na wote wanaohitaji msaada na huruma ya Baba Mtakatifu..

Padre Lombardi anasema, Mwenyeheri Paulo VI na Mtakatifu Yohane Paulo II wakati wa hija zao za kichungaji nchini Sri Lanka hawakubahatika kutembelea na kusali kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu wa Madhu, kielelezo cha upatanisho, umoja na mshikamano wa kitaifa. Kumbe, Baba Mtakatifu Francisko ametembelea na kusali katika Madhabahu haya yanayopendwa na waamini kutoka katika dini mbali mbali nchini Sri Lanka. Hapa wanajisikia kupendwa, kuthaminiwa na kuheshimiwa.

Katika Madhabahu haya, Baba Mtakatifu ametafakari kwa kina kuhusu umuhimu wa upatanisho, toba na msamaha wa kweli, ili kuvuka kinzani na migawanyiko inayotokana na tofauti za kidini, kisiasa, kitamaduni na kikabila. Baba Mtakatifu amepokea Sanamu ya Bikira Maria na kuwabariki watu waliokuwa wamefurika katika Madhabahu haya.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu imechangia mchakato wa amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, tayari kuendeleza upatanisho wa kitaifa. Kanisa Katoliki nchini Sri Lanka limeonesha umahiri mkubwa katika kuandaa na kutekeleza hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu nchini humo na kwamba, Baba Mtakatifu ameridhika na mapokezi makubwa yaliyofanywa kwake, jambo ambalo limewasha cheche za matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.