Changamoto kubwa ni kuendeleza majadiliano ya kidini, maridhiano, haki na amani!
Kardinali mteule Charles Maung Bo, Askofu mkuu wa Yangon, nchini Myanmar, atakaposimikwa
rasmi, hapo tarehe 14 Februari 2015, atakuwa ni Kardinali wa kwanza kutoka nchini
humo. Anasema, changamoto kubwa inayomkabili mbele yake ni kuendeleza mchakato wa
majadiliano ya kidini, maridhiano, haki na amani kati ya wananchi wa Mynmar.
Kanisa Katoliki
nchini humo linawakilisha idadi ndogo sana ya wananchi wa Mynmar na kwamba, kwa sasa
nchi yake iko katika kipindi cha mpito kuelekea kukua kwa demokrasia baada ya utawala
wa mabavu kutikisa nchi hiyo kwa miaka kadhaa. Kinzani za kisiasa zilipelekea kuibuka
kwa mgogoro wa kidini na kikabila, hali ambayo imesababisha kurasa chungu kwa wananchi
wa Myanmar.
Viongozi wa kidini anasema Kardinali mteule Bo, wanaweza kusaidia
kwa kiasi kikubwa kujenga msingi wa haki, amani, upatanisho na maridhiano kati ya
watu na kwamba, anapenda kuchukua fursa hii kuhakikisha kwamba, viongozi wa kidini
wanashrikiana kwa karibu zaidi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wao.
Ukosefu
wa haki msingi za binadamu na utawala wa sheria ni mambo ambayo yanapelekea kwa kiasi
kikubwa uwepo wa kinzani za kidini na kikabila, kwani kuna kundi la watu ambalo linaona
kwamba, halitendewi haki kama inavyostahili kadiri ya Katiba ya nchi ambayo kimsingi
ni sheria mama. Kwa sasa kuna muswada wa sheria ambao una taka kuzuia masuala ya ndoa
na uhuru wa kidini: changamoto kubwa katika kudumisha amani na utulivu! Na Padre
Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.