Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda amezindua rasmi Bodi ya Uongozi
ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na kuitaka bodi hiyo kufanya kazi zake kwa kuzingatia
sheria na kushirikiana na menejimenti ya chuo hicho kuweka mikakati na mipango ya
maendeleo itakayokiwezesha chuo hicho kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza
na viongozi na wajumbe wa bodi hiyo Jumanne, tarehe 13 Januari 2015 jijini Dar es
salaam, Dkt. Kigoda amesema serikali inayo imani kubwa na Mwenyekiti na wajumbe wa
Bodi hiyo walioteuliwa na kwamba watatimiza majukumu yao kikamilifu na kukiwezesha
chuo hicho kufikia malengo na matarajio ya watanzania ya kuendelea kuzalisha wataalam
bora wa fani za biashara.
“Ninaamini kuwa Bodi niliyoizindua leo itasimamia
shughuli za chuo hiki kwa kufuata misingi ya uadilifu,utawala bora na kuongeza chachu
ya kuleta huduma bora kwa wananchuo na umma” Amesisitiza Dkt. Kigoda.
Amesema
viongozi na wajumbe wa Bodi walioteuliwa wanalojukumu la kusimamia ustawi wa chuo
hicho wakiwa chombo cha juu cha utoaji wa maamuzi na usimamizi wa masuala mbalimbali
ya chuo hicho ikiwemo uidhinishaji wa matumizi ya chuo yanayoendana na mapato ya chuo,
uteuzi wa Mkuu wa Chuo na watumishi wengine na uidhinishaji wa viwango vya ada.
Akizungumzia
mabadiliko ya chuo hicho toka kuanzishwa kwake mwaka 1965 Dkt. Kigoda amesema yamehusisha
mabadiliko makubwa ya mitaala ya kufundishia ili kuwafanya wanafunzi na wahitimu waweze
kupanua ufahamu wao kwa kuwa na uwezo wa kukabiliana na ushindani wa soko la ajira
kwa kuongeza fursa za ajira katika sekta ya umma na binafsi pamoja kuwajengea uwezo
wahitimu waweze kujiajiri wenyewe.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Prof.
Emanuel Mjema akizungumza wakati wa kuwakaribisha wajumbe walioteuliwa chuo hapo amesema
kuwa, wao kama viongozi wa chuo hicho wataendelea kusimamia msingi wa kuanzishwa kwa
chuo wa kuendelea kuzalisha wataalam bora katika nyanja za biashara na sekta ya uendeshaji
viwanda nchini. Amesema kuwa wao kama menejimenti ya chuo hicho watashirikiana na
uongozi na wajumbe wa bodi iliyoteuliwa kusimamia rasilimali na miundombinu ya chuo
hicho ili kiendelee kutoa huduma bora kwa wanafunzi na wananchi wengi Zaidi kwa wakati.
Naye
Makamu mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi ya Chuo hicho Prof. Eleuther Mwageni akizungumza
kwa niaba ya uongozi na wajumbe wa bodi iliyoteuliwa amesema kuwa Bodi iliyoteuliwa
itatekeleza majukumu yote yaliyoanishwa kwa mujibu wa sheria.