Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kawaida cha Mwaka!
Ninayofuraha kubwa hivi leo tunapojiunga pamoja nawe kutafakari Neno la Mungu chakula
cha roho zetu. Dominika iliyopita tulisherehekea sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, sikukuu
ambayo ilitualika kurudia ahadi za ubatizo wetu, na hivi kujiweka tayari kusonga mbele
katika imani katika mwaka mpya.
Kama ilivyo
kawaida sikukuu hiyo hufunga kipindi cha Noel na kuanzisha kipindi cha kawaida cha
mwaka. Leo basi mpendwa tupo pamoja katika Dominika ya II ya mwaka.
Mpendwa
msikilizaji, Neno la Mungu katika Dominika hii latusaidia kugundua namna Mungu anavyoita
na namna gani tuitike. Kwa hakika Mungu humwita mtu kwa jina lake, ingawa huitwa kwa
mafaa ya jumuiya na Kanisa kwa upana wake kiulimwengu.
Hivi Mungu amfahamu
kila mmoja wetu kina, hakuna anayeweza kumdanganya Mungu. Mpendwa, Mungu aitapo huita
kwa uvumilivu, hachoki na hivi hutaka mpaka mtu asikie sauti yake, ndiyo kusema hushika
agano lake na msimamo thabiti katika ahadi zake. Mambo haya tunayajua kwa njia ya
wito wa Samueli. Anamwita kwa jina na polepole Samueli anasikia sauti ya Bwana.
Ewe
unayenisikiliza katika tafakari hii, sauti ya Mungu iitapo yadai kuitika na hivi Samueli
ni mfano bora wa namna ya kuitika akisema “nena Bwana kwa kuwa mtumishi wako anasikia”
Hii ndiyo sentensi ambayo wapaswa kuitamka kila siku ya maisha yako, tena ilingane
na moyo wa ndani.
Ni wajibu wa ubatizo ambao tuliupokea mwanzoni mwa imani
yetu na hata tukarudia ahadi za ubatizo katika sikukuu ya Ubatizo wa Bwana na kila
siku katika Kanuni ya imani. Mpendwa tunahitaji maongozi ya kimungu ili tuweze kusikia
vema sauti ya Mungu, na hivi kazi ya Eli aliyekuwa kuhani ilikuwa kumsaidia Samueli
apambanue sauti ya Mungu toka sauti nyingine.
Leo hii Kanisa zima latusaidia
kupambanua sauti ya Bwana. Mtakatifu Yohane Paulo II katika barua yake ya kichungaji
iitwayo “Familiaris Consortio” juu ya Wajibu wa Familia za Kikristo anawaalika mapadre
na wote wenye kushughulikia familia wakizingatia Maongozi ya Magisterium yaani mamlaka
ya Kanisa wapambanue yote yaliyo mema toka mabaya katika kuzielekeza familia kwenye
utakatifu. Katika hili, Kanisa lamwalika mmojammoja kuwa na mlezi wa kiroho anayesaidia
kuongoza maisha ya Kikristo.
Mtume Paulo atuonya kama alivyowaonya Wakorinto
kuwa mwili si kwa zinaa bali ni hekalu la Roho wa Bwana. Mwili ni zawadi kwa mwanadamu
kwa ajili ya uumbaji na hivi yatupasa daima kukumbuka kuwa tunaitwa kutunza na kuheshimu
mwili tuliokabidhiwa na Mungu. Kumbuka fumbo la umwilisho, Bwana alitaka kuutakatifuza
mwili na hivi katika mlengo huo nasi twafanya hivyo.
Katika somo la Injili
tunaalikwa katika wito tulioupokea kuwa kama Yohane Mbatizaji. Anamtambulisha Bwana
na kisha anamwacha Bwana asonge mbele na kazi yake. Utume wa Yohane ulikuwa wa kutayarisha
njia ya Bwana na sasa Bwana lazima akue na Yohane Mbatizaji apungue.
Je sisi
twawaalika watu kwenda kwa Kristu au kwa ajili yetu wenyewe ktk ubinafsi wetu?, tafakari!
Je twajiona wa maana zaidi kuliko wengine? Tunaalikwa basi hivi leo kutekeleza wito
wetu kwa njia ya fadhila ya unyenyekevu.
Mitume wanapoongea na Bwana na wanagundua
kuwa Bwana ni Masiha na wanasema tumemwona Masiha. Wanaitika na wanamwona Bwana kuwa
ni mwalimu wao yaani Rabbi. Je wewe wachukua muda kuongea na Bwana na kuonja upendo
wake na kujua ataka nini kwako au wakurupusha tu sala na maisha yako ya kiwito kwa
ujumla kiasi kwamba huoni Bwana ni nani? Mtume Andrea anampeleka kaka yake Simon Petro
kwa Yesu baada ya kujua kwamba Kristu ni Masiha, je sisi katika kutekeleza wito wetu
twawapeleka ndugu zetu kwa Bwana au kwa watu wengine?
Bwana anamwambia Simoni
Petro kuwa ataitwa Kefa yaani Petro au Mwamba! Anaanza kumtayarisha kwa kuwa mwamba
wa Kanisa, Je, wewe uko tayari kuwa mwamba wa upendo katika familia yako na mahali
pako pa kazi? Tafakari.
Mpendwa mwana wa Mungu ninakutakieni Dominika njema
ukajazwe na upendo wa Bwana uwe chumvi na mwanga kwa ajili ya wengine. Kwa njia yako
watu wamwone Mungu. Kwa njia ya matendo yako adilifu na unyenyekevu wako umwachie
nafasi Yesu Kristo akue na hivi polepole Neema za Mungu zienee kwa wote.
Tumsifu
Yesu Kristo. Kutoka katika studio za Radio Vatican ni Padre Richard Tiganya, C.PP.S.