Kardinali Malcolm Ranjith wa Jimbo kuu la Colombo, Sri Lanka anasema, Mtakatifu Joseph
Vaz alizaliwa huko Goa, Hindia kunako tarehe 21 Aprili 1651, hata katika ujana wake,
ni mwamini aliyejipambanua kwa maisha ya sala na tafakari ya kina, kwa kutumia muda
wake mwingi kwa ajili ya sala.
Alikuwa ni
msomi, aliyejisadaka kwa ajili ya kuwahudumia maskini na wote waliokuwa wanasukumwa
pembezoni mwa jamii; kwa kuwaoneha huruma na upendo wa Mungu katika hali ya unyenyekevu
pasi na makuu; alikuwa ni mtu wa furaha katika kuwahudumia watu; mambo yaliwagusa
watu kutoka katika undani wao, wengi wakauona utakatifu wa maisha yake tangu awali.
Baada
ya masomo na majiundo yake ya Kikuhani, akapewa Daraja takatifu la Upadre kunako mwaka
1676 akiwa ni Padre wa Jimbo kuu la Goa, India. Lakini ndani mwake, aliendelea kujisikia
kuwa na wito wa kuwa Mmissionari, tayari kutoka ili kuwatangazia watu Habari Njema
ya Wokovu, akamua kujiunga na na Shirika la Padre Pasqual dal Costa Jeremias; baadaye
akawa ni kiongozi na hatimaye wakajiunga na Shirika la Mtakatifu Filippo Neri. Akiwa
Jimbo kuu la Goa, akaanzisha Shirika lake binafsi, kwa kuendeleza sheria na kanuni
za Shirika la Mtakatifu Filippo Neri.
Padre Joseph Vaz alibahatika kufahamu
kwa undani mateso na mahangaiko ya Wakristo nchini Sri Lanka na kunako mwaka 1687
akaamua kwenda nchini humo kama mfanyakazi. Haikuwa rahisi kwake kukutana na Waamini
wa Kanisa Katoliki, lakini aliendelea kujifunza lugha ya kitamil, akahudumia waamini
katika hali ya kificho na baadaye Waholanzi walimshtukia na kuanza kumtafuta kwa udi
na uvumba, ili wapate kumwadabisha, kwani walimshutumu kuwa ni mpelelezi wa Wareno
waliokuwa wanatawala eneo hili kwa nyakati zile.
Siku moja akiwa njiani kwenda
kukutana na Mfalme wa kitongoji cha Kandy, alikamatwa na kutiwa kizuizini. Baada ya
miaka miwili aliachiliwa na kupewa kifungo cha nje na hivyo kuendelea na utume wake
kama mchungaji na kiongozi wa maisha ya kiroho, akachakarika kuwatangazia Watu Habari
Njema ya Wokovu sanjari na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa; akaonesha matendo makuu
ya Mungu katika maisha yake, kwa kufanya miujiza.
Alikataa katu katu alipoombwa
kuwa Askofu, akataka aendelee kuhudumia kama Padre. Mateso aliyopata awali na kuyakubali
kwa moyo wa unyenyekevu yalimsababishi maradhi makubwa na tarehe 16 Januari 1711 akafariki
dunia! Ni Padre aliyejisadaka na kumwachia Kristo aweze kuyaongoza maisha yake kama
alivyokuwa Yohame Mbatizaji katika Agano Jipya. Kunako mwaka 1713 cheche za mchakato
wa kumtangaza Padre Joseph Vaz kuwa Mwenyeheri zikaanza huko Goa na Kandy.
Kunako
mwaka 1989 Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu likatambua
ushuhuda wake wa imani na miujiza iliyotendwa kwa maombezi yake. Papa Yohane Paulo
II tarehe 21 Januari 1995 akatangaza kuwa ni Mwenyeheri, wakati wa hija yake nchini
Sri Lanka.
Waamini na watu wenye mapenzi mema kutoka ndani na nje ya Sri Lanka
waliendelea kusali kwa maombezi ya Mwenyeheri Joseph Vaz na Baba Mtakatifu Francisko
kunako tarehe 20 Oktoba 2014 akaamua atangazwe kuwa Mtakatifu, tukio ambalo linafanyika
nchini Sri Lanka wakati wa hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko. Kanisa
linafurahi kwa kupata zawadi hii kubwa na linamshukuru kwa kuwaimarisha waamini katika
imani na kwamba, ataendelea kukumbukwa kama mmissionari hodari aliyejisadaka kwa ajili
ya kuwatangazia watu Injili ya Matumaini kwa Kristo na Kanisa lake.
Sri Lanka
ikawa ni chachu ya Uinjilishaji Barani Asia, kwa kuwa ni mahali pa kwanza kabisa Barani
Asia kuwa na Seminari kwa ajili ya majiundo ya Majandokasisi mahalia, tayari kujisadaka
kwa ajili ya kuwatangazia watu Injili ya Kristo. Papa Leo mkuu, aliwahamasisha viongozi
wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanawafunda waseminari kikamilifu, tayari kushiriki
katika mchakato wa Uinjilishaji wa watu Barani Asia.
Ukuu wa Mwenyeheri Joseph
Vaz unafumbatwa katika maamuzi yake ya kujisadaka kwa ajili ya upendo na huduma kwa
ndugu zake katika Kristo waliokuwa wanateseka bila ya kuwa na mchungaji; ni mwamini
aliyejiachilia mikononi mwa Mungu, kwa ajili ya huduma kwa maskini; akaonesha ukuu
wa maisha ya sala na tafakari ya Neno la Mungu; akaadhimisha Mafumbo Matakatifu kwa
Ibadan a moyo mkuu, chemchemi ya utakatifu wa maisha na ukuu wa Mungu kwa watu wake.
Kwa hakika ni Joseph Vaz ni Mmissionari wa kuigwa katika mchakato wa Uinjilishaji
Mpya, changamoto kubwa inayofanyiwa kazi na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia
ya tatu ya Ukristo.
Wakristo Barani Asia hawana wasi wasi tena wa kuteseka
kutokana na umaskini wala madhulumu, wanachohitaji ni Wamissionari wanaojisadaka kwa
ajili ya kuwatangazia watu Injili ya Furaha na Matumaini kwa Kristo na Kanisa lake,
ili Kristo aendelee kufahamika pasi na makuu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.