2015-01-14 10:05:56

Mapambano dhidi ya umaskini yanalenga kupunguza mpasuko wa kijamii!


Rais Maithripala Sirisena, katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini Sri Lanka, Jumanne, tarehe 13 Januari 2015 amesema kwamba, ni fursa ya kupata baraka na neema anapoanza uongozi wake kama Rais wa Sri Lanka.

Imegota miaka ishirini tangu Papa Yohane Paulo II alipotembelea Sri Lanka wakati huo ikiwa imegubikwa kwa vitendo vya kigaidi vilivyoonekana kuwa kama sehemu ya maisha ya watu, lakini leo hii, mambo yamebadilika amani na maendeleo yanaendelea kushika kasi, watu wanafurahia maisha ambayo ameboreka kwa kiasi kikubwa. Lakini changamoto kubwa ni mapambano dhidi ya umaskini, ambao kwa sasa yamepewa kipaumbele cha kwanza na serikali, ili kupunguza mpasuko wa kijamii kati ya maskini na matajiri.

Hija ya Baba Mtakatifu nchini Sri Lanka anasema Rais Sirisena inafanyika wakati ambapo Serikali imeanzisha mchakato wa majadiliano na upatanisho kati ya watu, ili kujenga na kuimarisha amani; kwa kuendelea kujikita karika maridhiano ya watu wa dini mbali mbali kama sehemu ya utajiri na urithi mkubwa wa wananchi wa Sri Lanka. Serikali inampongeza Baba Mtakatifu kwa juhudi zake za upatanisho katika medani za kimataifa.

Rais Sirisena anapongeza mchango uliotolewa na Mtakatifu Joseph Vaz katika kuimarisha imani, upatanisho, ustawi na mapendo kati ya watu, licha ya tofauti zao za kidini. Hii ni changamoto kubwa inayopaswa kufanyiwa kazi na waamini wa dini mbali mbali katika mchakato wa kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini, ili amani, utulivu, maridhiano na udugu viweze kushika kasi, kama anavyokazia Baba Mtakatifu mwenyewe katika ujumbe wake kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.