Tanzania imesema kuwa ni jambo la kusadikika na kufikirika tu kwa baadhi ya watu kudai
kuwa haiko tayari kukabiliana na vikundi vya uasi na ugaidi (negative forces) vilivyobakia
vikivuruga amani na kusababisha ukosefu wa utulivu ndani ya nchi jirani ya Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Badala yake, Tanzania inaendelea kuwa tayari
kukabiliana na vikundi hivyo, kwa mujibu wa mamlaka ambayo majeshi yake pamoja na
yale ya Afrika Kusini na Malawi, yamepewa na Umoja wa Mataifa (UN) ya kuvishambulia,
kuvimaliza nguvu na kuvinyang’anya silaha (neutralize and disarm all negative forces)
vikundi hivyo vyote.
Nchi hizo tatu zinaunda Brigedi ya Kimataifa ya Force
Intervention Brigade (FIB), ambayo ni sehemu ya Majeshi ya UN katika DRC ya United
Nations Stabilisation Mission in Congo (MONUSCO), yaliyoko chini ya Luteni Jenerali
Alberto Santacruz wa Brazil. Chini ya mamlaka ambayo Brigedi hiyo imepewa na UN, majeshi
ya nchi hizo tatu, yana uhalali wa kuvishambulia vikundi vya kiasi katika DRC.
Msimamo
huo wa Tanzania umerudiwa tena na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete, Jumanne, Januari 13, 2015, alipokutana na kufanya mazungumzo
na Mheshimiwa Novisise Mapisa-Nqakula, Mjumbe Maalum wa Rais wa Afrika Kusini na Waziri
wa Ulinzi wa nchi hiyo. Waziri Nqakula amefuatana na Waziri wa Usalama wa Afrika Kusini,
Mheshimiwa Mahlobo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati akiwatakia mabalozi
wanaoziwakilisha nchi zao katika Tanzania Heri ya Mwaka Mpya wakati wa Halfa ya Mwaka
ya Sherry Party iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, Rais Kikwete aliyaeleza maoni na
shutuma dhidi ya Tanzania kuwa ni mambo ya “kudharauliwa”. Katika mazungumzo hayo
yaliyofanyika Ikulu, Zanzibar, Rais Kikwete amemwambia Bibi Nqakula kuwa msimamo wa
Tanzania umekuwa ule ule wa siku zote bila mabadiliko yoyote – yaani kuhakikisha kuwa
majeshi na vikundi vyote vya uasi ndani ya DRC vinamalizwa. Rais Kikwete amekuwa Zanzibar
tokea Jumatatu, Januari 12, 2015 wakati alipohudhuria sherehe za miaka 51 ya Mapinduzi
ya Zanzibar.
“Wako watu wanaojidai kuwa na uwezo mkubwa wa kusoma na kuelewa
zaidi maoni na mtazamo wa Tanzania kuliko hata Tanzania yenyewe ….wanadai kuwa Tanzania
haina nia ya kukabiliana na vikundi vya uasi katika DRC. Ni watu wa ajabu kabisa hawa
kwa sababu Tanzania, kama zilivyo Afrika Kusini na Malawi, zina askari wake katika
DRC chini ya Mamlaka ya Umoja wa Mataifa,”amesema Rais Kikwete.
Ameongeza:“Tumeanza
kuifanya kazi iliyotupeleka huko kwa kukisambaratisha Kikundi cha M-23. Tuko tayari
kukabiliana na Kikundi cha FDLR (Democratic Forces for the Liberation of Rwanda) na
vikundi vingine kama vile ADF na vile vya mgambo kama vile Mai Mai. Kilichotuzuia
kuimaliza kazi hii mapema ni kwa sababu FDLR waliomba kujisamilisha wenyewe kwa hiari
na wakapewa miezi sita. Sasa muda huo umemalizika.”
Amesisitiza Rais Kikwete:
“Hivyo, tuko tayari kwa sababu bado majeshi yetu yako DRC na wala masharti ya UN ya
kushiriki katika Brigedia ya Kimataifa hayajabadilika na wala Serikali ya Tanzania
haijapeleka maelekezo tofauti kwa majeshi yake mbali na yale yaliyotolewa mwanzoni
mwa opereshani hiyo na UN.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Mamlaka ya ushiriki wa
majeshi yetu uko wazi, hakuna mchanganyiko wowote katika maelekezo yaliyotolewa kwa
askari wote na hakuna maelekezo mapya yaliyotolewa kwa vijana wetu. Wanaendelea na
kazi yao.”