2015-01-14 09:18:58

AMECEA inampongeza Kardinali mteule Souraphiel!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, linampongeza Askofu mkuu Berhaneyesus D. Souraphiel kwa kuteuliwa kwake na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Kardinali na kwamba, Familia ya Mungu kutoka katika nchi za AMECEA itaendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Kardinali, kwa ajili ya huduma kwa Kanisa la Kiulimwengu. RealAudioMP3

AMECEA inasema kwamba, Baba Mtakatifu ametambua mchango na huduma inayotolewa na Askofu mkuu Souraphiel kwa Jimbo kuu la Addis Ababa, Nchi za AMECEA na Afrika katika ujumla wake, ndiyo maana amemteua kuwa ni kati ya washauri wake wakuu kama Kardinali. AMECEA inatumia fursa hii kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko, kwa kutoa heshima kubwa kwa nchi za AMECEA na kwamba, wanamhakikishia sala na sadaka yao katika maisha na utume wake.

Salam na matashi mema zinatolewa pia na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki na Kati, CUEA ambacho Kardinali mteule Souraphiel ni mkuu wake. Makardinali wote walioteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko watasimikwa rasmi katika Ibada itakayofanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro hapo tarehe 14 Februari 2015.

Kardinali mteule Souraphiel anasema, anajiona kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amemnyanyua sana na kwamba, binafsi anajiona kuwa kamwe hastahili kupewa dhamana kubwa kiasi hiki kwa ajili ya Kanisa la Ulimwengu, lakini kwa neema na baraka za Mwenyezi Mungu anaipokea heshima hii na kwamba, yuko tayari kulihudumia Kanisa kwa moyo, akili na sala zake.

Anatambua kwamba, Kiongozi mahiri na mkuu wa Kanisa ni Yesu Kristo mwenyewe, wengine wanatekeleza dhamana aliyowakabidhi, kama wafanyakazi wasiokuwa na faida, wanaotekeleza mapenzi ya Kristo mwenyewe. Kardinali mteule Souraphiel anawaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Kardinali!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.