Askofu Paul Abel Mamba wa Jimbo Katoliki Ziguinchor, Senegal anasema, watu wanasubiri
kwa hamu na shauku kubwa mchakato wa amani utakaowawajibisha wahusika wa vurugu na
kinzani nchini Senegal kuweka silaha zao chini na kuanza majadiliano katika ukweli,
uwazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Senegal.
Tangu mwaka
1982 kuna makundi yanapigana huko Casamance ili kujitenga na Senegal. Askofu Paul
Abel Mamba katika salam na matashi mema ya Mwaka mpya 2015 alizowaandikia viongozi
wa Serikali katika Jimbo lake, amewataka viongozi hao kuhakikisha kwamba, amani, utulivu
na maendeleo ya wengi huko Casamance yanapewa kipaumbele cha kwanza katika ajenda
za kisiasa kwenye ngazi ya kitaifa kwa mwaka 2015.
Katika kipindi cha miaka
miwili iliyopita, makundi haya anasema Askofu Mamba yameendelea kukwamisha mchakato
wa majadiliano ili kupata amani ya kudumu. Kwa sasa hakuna vita wala watu hawana uhakika
wa usalama wa maisha na mali zao. Umefika wakati kwa wadau wakuu kuachana na ubinafsi,
uchu wa mali na madaraka, ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa amani, utulivu sanjari
na ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa kwani ukabila na umajimbo ni mambo ambayo
yamepitwa na wakati kwa sasa!