2015-01-13 07:56:44

Salam na matashi mema kutoka kwa Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko, akiwa njiani kuelekea Sri Lanka na Ufilippini wakati wa ziara yake, aliyoianza Jumatatu usiku, tarehe 12 Januari 2015, amewaandikia ujumbe wa matashi mema marais wa Italia, Albania, Ugiriki, Uturuki, Iran, Umoja wa Falme za Kiarabu, Oman na India.

Baba Mtakatifu amewatakia wakuu hao wa nchi pamoja na wananchi wao amani, usalama na ustawi sanjari na kuwapatia baraka zake za kitume. Amewahakikishia Marais hao sala na maombezi yake na kuwaomba hata wao kumsindikiza kwa sala na sadaka zao katika hija yake ya kitume huko Sri Lanka na Ufilippini. Baba Mtakatifu anawatakia wananchi wote ambao ndege yake imebahatika kuruka katika anga lao, amani na furaha.

Kwa namna ya pekee, amewaambia wananchi wa Uturuki kwamba, bado moyoni mwake kuna kumbu kumbu ya hija ya kichungaji aliyoifanya nchi mwao hivi karibuni na kwamba, bado anaendelea kuwakumbuka kwa sala! Baba Mtakatifu amewatakia wananchi wa Iran, Falme za Kiarabu na Omani, amani na ustawi, kama ambavyo pia amefanya kwa Rais wa India.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.