2015-01-13 07:39:47

Ni hija ya urafiki, majadiliano na mshikamano!


Baba Mtakatifu Francisko alianza maandalizi ya hija yake ya kitume nchini Sri Lanka na baadaye Ufilippini kwa kwenda kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma, Jumapili jioni na baadaye, Jumatatu usiku, tarehe 12 Januari 2015 aliondoka mjini Roma kuelekea Sri Lanka. Akiwa njiani, wakati huu, Baba Mtakatifu alipata nafasi ya kuzungumza na kila mwandishi wa habari aliyekuwa kwenye msafara wake pamoja na kubadilishana maneno mawili matatu!

Padre Federico Lombardi Msemaji mkuu wa Vatican anasema, wananchi wa Sri Lanka wamempokea Baba Mtakatifu Francisko kwa shangwe na vigelegele na kwamba, hotuba ya Bwana Maithripala Sirisena Rais wa Sri Lanka ilikuwa fupi sana kuliko ilivyotarajiwa kwani anasema kwamba, ameingia madarakani siku chache na kwamba, ujio wa Baba Mtakatifu nchini Sri Lanka ni tukio kubwa ambalo litaacha chapa ya kudumu katika uongozi na maisha ya wananchi wa Sri Lanka katika ujumla wao.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa ajili ya makaribisho nchini Sri Lanka, Jumanne, tarehe 13 Januari 2015, amesifia uzuri wa Sri Lanka unaojionesha kwa namna ya pekee si tu kwa uzuri wa hali ya hewa bali pia utajiri unaofumbatwa katika utofauti unaojikita katika tamaduni na dini zilizopo nchini Sri Lanka. Baba Mtakatifu amempongeza Rais mpya wa Sri Lanka kwa kuchaguliwa kwake kuwaongoza wananchi wa Sri Lanka. Amewashukuru viongozi mbali mbali wa kidini waliofika kumpokea anapoanza hija yake ya kitume nchini Sri Lanka.

Baba Mtakatifu anasema, hii ni hija ya kitume inayojikita katika mikakati ya shughuli za kichungaji, ili kuwaimarisha Wakatoliki nchini Sri Lanka pamoja na kusali nao. Kilele cha hija yake nchini Sri Lanka ni adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu, kwa ajili ya kumtangaza Mwenyeheri Joseph Vaz kuwa Mtakatifu; kielelezo makini cha upendo, heshima, maridhiano kati ya watu bila ubaguzi kwa misingi ya kikabila wala kidini.

Baba Mtakatifu anasema, hija hii pia ni kielelezo cha upendo na wasi wasi wa Kanisa kwa ajili ya watu wote pamoja na shauku ya Jumuiya ya Wakatoliki kushiriki kikamilifu katika mustakabali wa maisha na maendeleo ya Sri Lanka katika ujumla wake. Dunia ya leo imesheheni vita kati ya jumuiya; inakosa uwezo wa upatanisho wa tofauti na kinzani mpya na zile za zamani; kati ya makabila na dini; mambo ambayo hatimaye, yanasababisha vita.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Sri Lanka kwa miaka kadhaa imeathirika sana kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe na leo hii inatafuta mbinu ya kuganga na kuponya madonda kwa kujiimarisha katika msingi wa amani. Si rahisi kujiondoa kutoka katika hali ya ukosefu wa haki, chuki na uhasama; mambo ambayo yamerithiwa kwa miaka mingi na hivyo kuwa ni sababu ya vita. Mchakato wa uponyaji unahitaji haki na umoja wa kitaifa.

Katika mchakato wa upatanisho anasema Baba Mtakatifu, dini mbali mbali nchini Sri Lanka zina nafasi ya pekee na kwamba, jamii nzima ya wananchi wa Sri Lanka haina budi kuwa na sauti moja sanjari na kufanya kazi kwa njia ya ushirikiano. Kila mtu anapaswa kuwa huru ili kuchangia maoni, matumaini, mahitaji na wasi wasi unaojikita katika undani wa maisha yao. Yote haya yafanyike kama inavyopaswa kutendeka ndani ya familia; kwa kukubaliana, kuheshimiana hata katika tofauti msingi; mambo ambayo yanaweza kuwa kweli ni utajiri mkubwa kwa jamii.

Baba Mtakatifu anasema, pale ambapo watu wanajenga utamaduni wa kusikilizana kwa unyenyekevu, ukweli na uwazi, hapo kunaweza kuibuka tunu msingi na matarajio ya wengi. Kutokana na mwelekeo huu, mchakato wa upatanisho hauna budi kugusa miundo mbali mbali ya kijamii, ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu; kwa kuzingatia haki msingi za binadamu pamoja na kuhakikisha kwamba, kila mwanajumuiya anashirikishwa kikamilifu katika jamii.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, viongozi wa kisiasa, kidini na wasomi nchini Sri Lanka wataweza kupima maneno na matendo yao kwa ajili ya mafao ya wengi na kama sehemu ya mchakato wa uponyaji ujao na mchango makini katika ujenzi wa maendeleo ya wananchi wa Sri Lanka: kiroho na kimwili. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawatakia wananchi wote wa Sri Lanka kwamba uwepo wake nchini humo, uwe ni chemchemi ya urafiki, majadiliano na mshikamano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.