2015-01-13 12:17:52

Angalieni changamoto za kiimani na kimaadili Barani Ulaya!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliowaandikia washiriki wa mkutano wa Marais wa Tume za Maaskofu Katoliki kuhusu Mafundisho Tanzu ya Kanisa unaofanyika mjini Esztergom, Hungaria, amelipongeza na kulishukuru Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kwa kumpatia nafasi ya kukazia umuhimu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Mahalia, lakini kwa namna ya pekee, Tume za Maaskofu za Mafundisho Tanzu ya Kanisa, katika utekelezaji wa dhamana ya kujenga na kudumisha umoja na imani, sanjari na kuwarithisha vijana wa kizazi kipya.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kudumisha, kuimarisha na kumwilisha urika wa Maaskofu kama wanavyokazia Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, mkutano huu utawasaidia wahusika kufanya upembuzi wa kina na mapana kwa kuangalia mafundisho na mikakati ya shughuli za kichungaji inayokabiliwa na changamoto na matatizo makubwa katika uhalisia wa maisha Barani Ulaya, kwa kukazia umuhimu wa Injili ya Uhai, kwani bila hiyo, Bara la Ulaya linaweza kupoteza moyo wa ubinadamu ambao linaupenda na kuulinda.

Ujumbe huu wa Baba Mtakatifu Francisko umesomwa kwa niaba yake na Kardinali Gerhard L. Muller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa anayesimamia na kuratibu mkutano huu.







All the contents on this site are copyrighted ©.