2015-01-12 08:15:36

Lindeni Injili ya Uhai!


Kardinali Ricardo Ezzati Andrello, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Santiago del Cile, lililoko nchini Chile, ameukumbusha umati mkubwa wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za Chile, uliokuwa uliokuwa unashiriki katika utume wa vijana ndani ya Kanisa kwamba, maisha ni zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu; hii ni zawadi ambayo mwanadamu anapaswa kulinda, kuitunza na kuindeleza, dhidi ya utamaduni wa kifo!

Hii ndiyo haki msingi na nguzo ya haki nyingine zote ambazo mwanadamu anapaswa kupewa na jamii! Hakuna haki pasi na maisha anasema Kardinali Ezzati Andrello. Amewaambia vijana kutoka Chuo kikuu cha Kipapa cha Kikatoliki nchini Chile kwamba, Serikali ina mpango wa kuandaa muswada wa sheria utakaoruhusu wanawake waliobakwa au wanawake wajawazito ambao afya yao iko hatarini kutoa mimba.

Kardinali anasema, Kanisa linasadiki na kufundisha kwamba, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, kila mtu anapaswa kulinda, kuitunza na kuiendeleza. Katika Ibada ya Misa takatifu, Kardinali Ezzati Andrello ameonesha wasi wasi na mashaka kuhusiana na mchakato unaotaka kuanzishwa na Serikali kuhusu mabadiliko katika mfumo wa elimu na kwamba, mchakato huu kwa vyovyote vile unapaswa kuwa ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi na wala si propaganda za kisiasa ambazo ni hatari kwa maendeleo ya elimu.

Mabadiliko yazingatie kwanza kabisa dhamiri nyofu, akili na hekima ya kufundishia, ili kuwasaidia wanafunzi kukua na kukomaa. Kardinali kwa namna ya pekee kabisa amewashukuru na kuwapongeza vijana kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Kanisa linapowatia dhamana ya kwenda kuwatangazia vijana wenzao Injili ya Furaha na Matumaini; changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu.

Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajenga na kuimarisha upendo, mshikamano na udugu kati ya watu, kwa kushirikishana furaha na karaha, ili kwa njia ya mchakato huu, watu wengine waweze kuonja cheche za imani na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Michezo, nyakati za mapumziko na mikutano ya vijana katika ngazi mbali mbali, iwe ni fursa ya kushirikisha cheche za imani na matumaini miongoni mwa vijana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.