2015-01-12 08:35:32

Karibu nchini Sri Lanka


Kardinali Malcolm Ranjith wa Jimbo kuu la Colombo, Sri Lanka anasema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Asia, lakini kwa namna ya pekee kabisa nchini mwake ni zawadi kubwa kwa familia ya Mungu nchini humo pamoja na kuwapatia zawadi ya kumtangaza Mwenyeheri Joseph Vaz, kuwa Mtakatifu, hapo Jumatano tarehe 14 Januari 2015.

Huu ni mwaliko ambao Baba Mtakatifu Francisko alipewa mara tu baada ya kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa Katoliki na akaupokea kwa moyo na unyenyekevu mkuu, ili kuwaonjesha waamini Barani Asia, upendo na mshikamano wa Mama Kanisa, hata katika uchache wao, kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa na Kanisa.

Mwaliko huu baadaye, ulitolewa rasmi na Baraza la Maaskofu Katoliki Sri Lanka kunako tarehe 3 Mei 2014 na hapo mwaliko ukawa rasmi. Hija hii ya kichungaji inapania kumwonesha Baba Mtakatifu Francisko imani, matumaini na mapendo yanavyomwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa Barani Asia, kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini na kitamaduni, kwa pamoja wakipania kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mafao ya wengi, kwani wote wanaunda Familia ya Mungu.

Kardinali Ranjith anasema kuna idadi kubwa ya Wakristo kutoka Barani Asia, huu ni utajiri mkubwa kwa maisha na utume wa Kanisa mintarafu kanuni maadili, tasahufi na ibada pamoja na kukumbuka kwamba, ni watu wenye historia na falasafa ya maisha, tofauti kabisa na watu kutoka sehemu nyingine za dunia.

Hija hii pamoja na mambo mengine, itaimarisha mchakato wa Uinjilishaji Mpya, dhamana inayovaliwa njuga na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu, pamoja na kujionea mwenyewe ushuhuda wa imani, inayomwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa, kama ilivyokuwa kwa Mwenyeheri Padre Joseph Vaz.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.