2015-01-11 12:54:39

Papa abatiza watoto 33: wazazi lisheni watoto pia na Neno la Mungu


Jumapili kwa ajili ya maadhimisho ya Siku Kuu ya Ubatizo wa Bwana, ikiwa pia ni kufunga kipindi cha Siku Kuu ya Noeli, Baba Mtakatifu Francisco ameadhimisha Ibada ya Misa katika Kanisa dogo la Sistine la mjini Vatican ,na ambamo pia amebatiza watoto 33 wa wafanyakazi wa Vatican. Watoto hao, wakiwa wanaume 12 na wasichana 21.

Katika mahubiri yake, Papa amewataka wazazi na wasimamizi, kuelea watoto katika mwanga wa Neno la Mungu. Na pia akatoa maombi kwa ajili ya akina mama wengi wasiokuwa na uwezo wa kulisha watoto wao, waweze kupata lishe kwa watoto wao.

Akitoa msisitizo kwa upande wa kiroho amesema kuwa ,ubatizo ni kuwekeza katika mwili wa Kanisa, ambao ni taifa la Mungu linalo tembea katika njia Takatifu. Na akakumbusha kwamba, haiwezekani kuwa Mkristo, nje ya kanisa. Na kwamba, Mwanga wa mshumaa unaowashwa kutoka Mshumaa wa fumbo la Pasaka, ishara ya Kristo Mfufuka, aliye hai kati yetu, hurithishwa mkono kwa mkono, kizazi hadi kizazi. Papa alirudia kuutaja urithi huu kwa mama, baba, wasimamizi wote wake kwa waume , kwamba , imani ya Kanisa ni watu wanaotembea katika njia ya imani, wakiirithisha imani yao kupitia ubatizo kwa watoto wao.

Papa aliendelea kuzungumzia juu ya imani ya kanisa akiangalisha pia katika imani ya Maria, Mama yetu, imani ya Mtakatifu Joseph, Mtakatifu Petro , Mtakatifu Andrea, Mtakatifu Yohana, imani ya Mitume na Mashahidi, ambayo inajidhihirisha kwa waamini kwa njia ya ubatizo. Papa amelitaja hili kuwa ni jambo jema, linaloonyesha mwanga wa Kanisa, ambao ni Mwili wa Kristo, watu wa Mungu , walio katika hija wakati wote na mahali popote, wakifundisha watoto wao kwamba, hawawezi kuurithi Ukristo wa wazazi bila ya ubatizo. Na hakuna anayeweza kuwa Mkristo nje ya Kanisa, na haiwezekani kuwa mfuasi wa Yesu Kristo bila Kanisa, kwa sababu Kanisa ni mama anayetufanya kukua katika upendo kwa ajili ya Yesu Kristo.

Na hivyo Papa aliwahimiza watu wazima Wakristo , hasa wazazi, wasimamizi, babu na bibi na ndugu wengine, kuwa mstari wa mbele kulisha Neno la Mungu, Injili ya Yesu, "chakula kikuu, cha familia, kinachoweza kukua na kuzaa matunda mazuri katika maisha, kama ilivyo mvua na theluji inyesha juu nchi, huiwezesha nchi kuzaa matunda. Neno la Mungu ni chakula bora, ambacho hutolewa na Mungu, Baba Mwema, na Mama mwema, mwenye kuwapa watoto wake, kilicho kizuri.

Papa amemshukuru Bwana kwa ajili ya zawadi ya maziwa ya mama na kuomba kwa ajili ya akina mama wengi, ambao kwa bahati mbaya, wameshindwa kuwa na chakula hiki kwa watoto wao. Papa ameomba uwepo wa uwezekano wa kuwasaidia akina mama hawa. Na akakumbusha kama yalivyo maziwa kwa mwili, Kiroho ndivyo ilivyo Neno la Mungu. Neno la Mungu hufanya imani kukua.

Papa ametoa wito kwa wazazi na wasimamizi na watu wazima ndani ya familia, wawe chemichemi ya maombi. Kumwomba Baba kwa ajili ya mahitaji ya familia na pia Roho Mtakatifu, daima awe mwalimu mwenye kuonyesha jinsi ya kuibeba familia , ili watoto waweze kukua na utambuzi wa uwepo wa nafsi ya tatu ya Utatu Mtakatifu, Roho mwenye kuongoza na kuvuvia kila siku yale tunayopaswa kufanya katika maisha yetu kama waamini. Papa amesali ili Roho Mtakatifu, aijaze mioyo ya waamini neema zake na kuwasha ndani yao moto wa upendo wa Mungu.








All the contents on this site are copyrighted ©.