Bwana Ban Ki-Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amesikitishwa na mauaji ya kinyama
yanayoendelea kufanywa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram nchini Nigeria kwa kusema
kwamba, kuna haja ya kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi;
watu kuvumiliana katika tofauti zao za kidini, kisiasa, kijamii na kitamaduni; kwa
kukazia ulinzi na usalama kwa watu na mali zao sanjari na kuendelea kuelimisha tabia
ya uungwana kati ya watu.
Katibu mkuu
wa Umoja wa Mataifa anasema, ni kwa njia hii, tu, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kupambana
vyema na changamoto ya vitendo vya kigaidi ambavyo vinaendelea kutishia usalama, maisha,
ustawi na maendeleo ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Dunia bado imepigwa na bumbuwazi
kutokana na mauaji ya kinyama yanayofanywa huko Iraq, Syria, Libia na Ufaransa. Viongozi
wa kidini wasimame kidete kupinga mauaji ya kinyama yanayofanywa na waamini wenye
misimamo mikali ya kiimani, kwani watu hawa ni hatari kwa usalama wa Jumuiya ya Kimataifa.
Katibu
mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kikao cha Baraza kuu la Umoja wa Mataifa ameitaka
Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika majadiliano na maridhiano kati ya watu, ili kujenga
na kuimarisha haki, amani na mshikamano, ili kushinda kishawishi cha vitendo vya kigaidi
ambavyo vinaendelea kuzua hofu na mashaka kati ya watu. Jumuiya ya Kimataifa inaweza
kulinda na kudumisha amani na utulivu, ikiwa kama haki msingi za binadamu zinaheshimiwa
na kuthaminiwa, bila kusahau uhuru wa kidini.
Wachunguzi wa mambo ya kisiasa
wanasema mashambulizi ya kigaidi yanayofunikwa kwa blanketi la misimamo mikali ya
kidini, lakini nyuma yake kuna masilahi ya kiuchumi, yanayochochewa sana na biashara
haramu ya silaha ambayo imekuwa ni chanzo kikuu cha vita na majanga yanayoendelea
kutokea sehemu mbali mbali za dunia.
Ugaidi ni jambo linalotishia maisha, usalama,
ustawi na maendeleo ya watu, jambo ambalo kwa sasa linavaliwa njuga na viongozi wa
Jumuiya ya Kimataifa. Jambo la kushangaza ni kuona kwamba, kuna idadi kubwa ya wananchi
kutoka katika nchi za Ulaya wanaojiunga na vikundi vya kigaidi ili kufanya mashambulizi
si tu katika nchi za kigeni hata katika nchi zao asilia. Jumuiya ya Kimataifa inaendelea
kuchukua tahadhari kubwa kuhusiana na vitendo vya kigaidi.