2015-01-09 12:11:46

Papa ni mjumbe wa majadiliano na upatanisho kati ya watu!


Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume Barani Asia anapenda kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini, kitamaduni na upatanisho kati ya watu; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; mambo msingi yatakayojiri kwenye hotuba zake kumi na moja anazotarajiwa kutoa nchini Sri Lanka na Ufilippini, wakati wa hija yake ya kitume kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 19 Januari 2015.

Kanisa katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita limeendelea kuwekeza zaidi Barani Asia, kama alivyotamani Mwenyeheri Paulo VI na Mtakatifu Yohane Paulo II, ili kujenga na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini, kitamaduni na upatanisho kati ya watu. Baba Mtakatifu akiwa nchini Sri Lanka anatarajiwa kumtangaza Mwenyeheri Joseph Vaz, kuwa Mtakatifu wa kwanza katika historia ya Kanisa nchini Sri Lanka, ikizingatiwa kwamba, Wakristo nchini humo wanaunda asilimia 7% ya idadi ya wananchi wote wa Sri Lanka. Lengo ni kuendelea kuwaimarisha Wakristo kuwa kweli ni Mashuhuda wa Kristo na Kanisa lake.

Ufafanuzi huu umetolewa hivi karibuni na Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anayebainisha kwamba, kauli mbiu ya hija ya Baba Mtakatifu nchini Ufilippini inajikita katika upendo na msamaha, kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 500 tangu Ukristo ulipoingia nchini Ufilippini.

Baba Mtakatifu anapenda kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo, hasa wanapoendelea kukabiliana na changamoto zinazotokana na majanga asilia ambayo yamekuwa ni chanzo kikuu cha maafa na umaskini kati ya watu.







All the contents on this site are copyrighted ©.