2015-01-09 11:12:10

Iweni wajenzi wa amani duniani!


Patriaki Cyrill wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow, nchini Russia, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli ambayo imeadhimishwa na Kanisa hili, usiku wa kuamkia tarehe 7 Januari 2015, amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushikamana kwa dhati ili kulinda, kutetea na kudumisha haki, amani na utulivu sehemu mbali mbali za dunia, kwa kutambua kwamba, hili ni jukumu la wengi.

Ibada hii imehudhuriwa na viongozi wakuu wa Serikali na kidini kutoka Russia. Katika salam zake za Noeli, Patriaki Cyrill amewataka watu wote wenye mapenzi mema kuwa kweli ni wajenzi wa amani kwa kuwashirikisha jirani zao ujumbe wa amani, unaopata chimbuko lake kutoka kwa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia. Ni changamoto ya kuondokana na vita, chuki na uhasama unaovuruga maisha ya watu wengi na badala yake kujikita katika haki, amani na upatanisho na hasa nchini Ucrain ambako bado mtutu wa bunduki unateketeza maisha ya watu wasiokuwa na hatia. Ulimwengu unahitaji amani na utulivu kama kikolezo cha maendeleo endelevu ya binadamu.

Patriaki Cyrill amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, hata katika tofauti zao za kiimani, kisiasa na kitamaduni, lakini wajitahidi kuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa amani. Wakristo kwa namna ya pekee kabisa wamepewa dhamana ya kuwashirikisha wengine amani inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, ili kuvuka vita, kizani na migogoro ambayo chimbuko lake ni dhambi, ubinafsi, uchoyo, tamaa ya mali na madaraka. Haya ni mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kanisa kwa upande wake, halichoki kuwatangazia Watu wa Mataifa Ujumbe wa furaha ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Mwakozi wa dunia, mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuamini na kungojea neema ya Mungu katika maisha yake; kwa kutafuta kumfahamu, kumpenda na kumtumikia, ili kudumisha mahusiano mema na kuwa walau sawa naye. Imani ya kweli iwawezeshe waamini kuwa waaminifu kwa Mungu na hivyo kuondokana na mawazo, maneno na matendo yanayosigana kimsingi na mapenzi ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Watu wajifunze kumpenda Mwenyezi Mungu na jirani yao, ambaye ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Wakristo wa Kanisa la Kiorthodox wanachangamotishwa kuwa kweli ni mashuhuda waaminifu wa imani inayomwilishwa katika matendo. Kipindi cha Noeli, ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujifunza kumpenda Mungu na jirani na kumhudumia Yesu Kristo kwa njia ya jirani, kwani wokovu ulioletwa na Yesu Kristo Mkombozi wa dunia ni kwa ajili ya wote na wala hakuna mtu anayetengwa na huruma pamoja na mapendo ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.