Huu si mchapo ni Neno! "Mara akatokea mle ndani ya Sinagogi mtu mmoja mwenye pepo
mchafu, akapaza sauti, 'Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza?
Najua wewe ni nani: wewe ni Mtakatifu wa Mungu!' Yesu akamkemea huyo pepo akisema,
'Nyamaza! Mtoke mtu huyu'. Basi, huyo pepo mchafu akamtikisatikisa mtu huyo, kisha
akalia kwa sauti kubwa, akamtoka. (Marko 1:23-26).
Hapa tuona nguvu ya Yesu
katika kugusa na kurekebisha maisha yetu. Yesu huyo ambaye hivi karibuni tumempokea
katika maadhimisho ya Noeli na kusema "Mtoto amezaliwa kwa ajili yetu, tumepewa mtoto
mwanaume mwenye uweza wa kifalme mabegani mwake".
Huyu ndiye Yesu aliyejidhihirisha
kwa Mamajusi kutoka Mashariki ya Mbali, waliomtambua na kumsujudia, huku wakimtolea
zawadi zao. Yesu ni mfalme wa amani, matumaini na mapendo; ni Mfalme mwenye uweza
mkuu kwa hiyo tusiishie kumkaribisha tu kwa maneno, kwa nyimbo, kwa kumlia pilau na
kumnywea soda na “viroba” Wala siyo kwa kumvalia nguo mpya kama tufanyavyo tunaposherekea
kuzaliwa kwa Yesu, bali tumkaribishe kwa dhati maishani mwetu ili asafishe tabia zetu
chafu ambazo sisi zimetushinda na tumezizoea na kuzifanya sehemu muhimu ya maisha
yetu.
Tabia hizo mbaya ndiyo pepo wachafu ambao wao wanamtambua Yesu na wanatambua
uweza wake, wanamwogopa. ulevi, ulafi, uzinzi, uongo, uvivu, chuki, hasira, kukata
tamaa, nguvu za giza, kutokushiriki mambo matakatifu, unafiki, undumilakuwili, kutokuwatendea
haki wenzetu, rushwa, kupenda anasa na fahari zote za kishetani, kutotimiza wajibu
na nyingine nyingi ni pepo wachafu ambao sisi tumewapa nafasi katika maisha yetu ya
kila siku, ni tabia ambazo zimetuzoea hatuna nguvu nazo. Ni tabia ambazo zinatufarakanisha
katika familia zetu, makazini na katika jamii.
Hizi ni tabia ambazo badala
ya kutupa furaha zimekuwa karaha kwetu, hatuna uwezo nazo, zinatuendesha. Leo tunapata
jibu, huyo mfalme mwenye uweza ndiye jibu kubwa, tuzitafakari tabia zetu, ambazo zinatukosesha
malengo yetu na zinatukosesha pia ya mbingu. Nguvu hizi za pepo wachafu hazina nguvu
mbele ya Yesu.
Tumuombe huyu 'mtoto aliyezaliwa kwa ajili yetu' ili atuondolea
'mizigo hiyo' inayotuelemea katika maisha yetu ili tuanze vyema mwaka huu tukiwa bila
pepo wachafu.
Tumsifu Yesu Kristo! Na Antipasi Shinyambala, Jimbo kuu
la Dar es Salaam.