2015-01-08 12:01:14

Monsinyo Joèl Marcier ateuliwa kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Wakleri


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Monsinyo Joèl Mercier, kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Wakeri na hivyo kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu mteule Joèl Mercier alikuwa ni Afisa mwandamizi katika Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu.

Askofu mkuu mteule Joel Mercier alizaliwa tarehe 5 Januari 1945 huko Chaudefonds-sur- Layon, Jimboni Angers, Ufaransa. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 27 Juni 1970 akapewa Daraja Takatifu la Upadre, Jimboni Angers. Kuanzia mwaka 1971 hadi mwaka 1974 alijiendeleza kwa masomo na juu na hatimaye kujipatia Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa, kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, kilichoko mjini Roma.

Kwa miaka kadhaa alikuwa ni Paroko msaidizi, Mlezi wa Waamini walei Jimboni Angers, Katibu muhtasi wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Angers na mjumbe wa Mahakama ya Kikanisa ya Jimbo la na Jaalimu wa Sheria za Kanisa katika Kitivo cha Taalimungu, Chuo Kikuu cha Angers. Kuanzia mwaka 2002 aliteuliwa kuwa Afisa mwandamizi wa Baraza la Kipapa la Maaskofu na mwaka 2007 aliteuliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kuwa Baba wa maisha ya kiroho kwa Majandokasisi kutoka Ufaransa wanaosoma na kufundwa mjini Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.