Maimamu wa Kifaransa mjini Vatican, ishara ya urafiki na majadiliano
Watu sita walionusurika katika kambi za mateso ya Auschwitz na maimamu wanne toka
Ufaransa, walikuwa kati ya umati mkubwa wa watu waliohudhuria katekesi ya Papa Francisko
, Jumatano ya wiki hii mjini Vatican. Kukutana kwao na Papa kumetajwa kuwa ushuhuda
dhahiri wa Wakatoliki na Waislamu, kupania kutembea pamoja katika hatua za kujenga
urafiki na maelewano, kama haja ya kidharura kwa ajili ya udumishaji amani na dhamira
ya kupambana na unyanyasaji wowote.
Maimamu hawa wanne, ni wajumbe wa miaka
mingi katika vikao vya pamoja vya Wakatoliki na Waislamu nchini Ufaransa, vikao vyenye
kuwa na lengo la kufanya kazi wa ushirikiano, kwa ajili ya kukuza majadiliano halisi
kati ya Wakatoliki na Waislamu. Ameeleza Askofu Michel Dubost wa Jiobo la Evry-Corbeil
–Essonnes , ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kwa
ajili ya Mahusiano na Madhehebu mengine. Anasema, kufahamiana husaidia kujenga mahusiano
ya kirafiki na hivyo hurahisisha kupata majawabu yanayofaa panapojitokeza changamoto
ngumu, kati ya waamini wa dini hizi mbili.
Na ameitaja ziara ya uwakilishi
huu wa Waislam kutembelea Vatican , kuwa si kitendo cha kipekee, lakini ni ishara
nzuri ya utendaji wa kazi zao za pamoja kwa ajili ya ujenzi wa amani. Hii ilikuwa
ni mara ya kwanza kwa uwakilishi wa juu wa Waislamu wa Ufaransa, kukutana na Papa
Francisco. Na kwamba, kazi za majadiliano yao, hulenga kuwaongoza katika njia ya
kupata majawabu, hasa jinsi ya kushughulikia mizizi ya ubabe wa kupindukia wa kidini,
uzuri wa kuvumiliana , na kujaribu kutoa majibu kwa mvutano wa kutisha unapojitokeza
kati ya madhehebu na dini, hali inayoonekana sehemu nyingi za Ulaya, lakini pia suala
nyeti Mashariki ya Kati.
Askofu Dubost aliwatambulisha Maimmu hao kwa Papa.
Nao ni Azzedine Gaci, gombera wa msikiti Orhman wa Villeurbanne, Maalim Tareq Oubrou,
gombera wa Msikiti Mkuu wa Bordeaux, mwingine ni Mohammed Moussaoui rais wa Umoja
wa misikiti nchini Ufaransa, na Djelloul Seddiki ambaye ni mkurugenzi wa Msikiti
Mkuu wa Al Ghazali wa Paris. Pamoja nao alikuwepo pia Padre kuhani Christophe Roucou,
Mkurugenzi katika Tume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kwa ajili ya mahusiano
na Uislamu.
Ujumbe huu wa Kiislam toka Ufaransa umekuwa Roma kwa ajili ya
kushiriki katika mfululizo wa mikutano ya ngazi ya juu, inayokamilika Alhamisi hii
8 Januari 2015, kwa kukutana na Kardinali Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili
ya Majadiliano ya kidini.