2015-01-08 08:03:03

Huruma na upendo!


Kila mwaka ifikapo tarehe 9 Januari, Wakristo nchini Ufilippini wanafanya maandamano makubwa ya Njia ya Msalaba na maandamano ya Mwaka 2015 yanajikita katika huruma na upendo unaofumbatwa katika maisha na utume wa Kanisa, kielelezo cha kauli mbiu inayoongoza hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Ufilippini. Hili ni tukio ambalo linawakusanya mamillioni ya waamini kutoka sehemu mbali mbali za Ufilippini ili kushiriki, baadhi yao wakiwa na imani kwamba, wanaweza kutendewa miujiza katika maisha yao!

Mapokeo yanaonesha kwamba, Maandamano ya Njia ya Msalaba, tukio la pekee kitaifa yanapata chimbuko lake kunako karne ya kumi na saba, kutoka Barani Asia. Yesu anayebebeshwa Msalaba mzito ni Ibada ambayo ilianzishwa na kunako mwaka 1606 na Padre mmoja wa Shirika la Waagostiani, kutoka Mexico, wakati huo, Ufilippini ilikuwa chini ya utawala wa Wahispania. Meli iliyokuwa imebeba Sanamu hii, iliungua moto kabla ya kutua nanga banadarini, lakini Sanamu ya Yesu Msalabani, ikasalimika kwa muujiza.

Kanisa Katoliki kwa kuthamini mapokeo na imani ya wananchi wa Ufilippini lilitoa kibali na kwamba, waamini wanaoshiriki katika tukio hili, kwa imani pamoja na kutimiza masharti yaliyowekwa na Kanisa, wanaweza kupata rehema kamili! Takwimu zinaonesha kwamba, maandamano haya ya Njia ya Msalaba kwa mwaka 2014, zaidi ya waamini millioni kumi!








All the contents on this site are copyrighted ©.