2015-01-08 08:27:00

Baa la njaa na umaskini ni vikwazo vikuu vya maendeleo ya binadamu!


Malengo ya Maendeleo ya Millenia kufikia Mwaka 2015 yaliyowekwa na Jumuiya ya Kimataifa, yalipania kuhakikisha kwamba, baa la njaa na umaskini linapunguzwa kwa kiasi kikubwa; watoto wenye umri wa kwenda shule wanapata fursa ya kuanza masomo ya msingi; kuhakikisha kwamba, idadi ya vifo vya wanawake wajawazito na watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano vinapunguzwa; sanjari na kuendelea kupambana na ugonjwa wa Ukimwi, Malaria na Kifua Kikuu.

Malengo ya Maendeleo ya Millenia yalitiwa mkwaju na wakuu wa Serikali 191 kunako mwaka 2000 ili kuonesha mshikamano kati ya nchi tajiri duniani na nchi zinazoendelea katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, usawa na maendeleo ya wengi. Wachunguzi wa mambo wanaangalia kwa jicho la udadisi kuona ni kwa jinsi gani Jumuiya ya Kimataifa itakuwa imefikia malengo haya ifikapo tarehe 31 Desemba 2015.

Bwana Massimo Caneva, mtaalam wa masuala ya ushirikiano wa kimataifa na mambo ya kibinadamu kutoka Italia anabainisha kwamba, bado kuna pengo kubwa kati ya nchi maskini na nchi tajiri zaidi duniani; bado kuna watu billioni moja wanaoandamwa na baa la njaa na utapiamlo, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya upembuzi yakinifu na kuangalia ni kwa jinsi gani Malengo ya Maendeleo ya Millenia yanaweza kutekelezwa kwa ajili ya mafao ya wengi, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, tunu msingi pamoja na kuendeleza mikakati ya elimu.

Tayari imekwishagota miaka kumi tangu Jumuiya ya Kimataifa ilipojiwekea Malengo ya Maendeleo ya Millenia! Lakini leo hii, kuna haja ya kuangalia pia masuala ya mabadiliko ya tabianchi ambayo kimsingi yamekuwa ni chanzo cha majanga makubwa kwa watu wengi duniani, kiasi cha kuathiri hata mafanikio yaliyopatikana katika miaka kumi iliyopita.

Kinzani za kidini na kijiografia ni changamoto ambazo zinapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa na Jumuiya ya Kimataifa, ili kujenga vijana wa kizazi kipya wenye uwezo wa kutatua matatizo na changamoto kwa njia ya majadiliano badala ya kukimbilia kwenye mtutu wa bunduki; watu wenye uwezo wa kudhibiti vita na kinzani za kijamii na kisiasa.

Bwana Massimo Caneva anakiri kwamba, kumekuwepo na mafanikio makubwa katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia kwa nchi nyingi duniani. Bara la Afrika linapaswa bado kuangaliwa kwa jicho la mshikamano katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi na mapambano dhidi ya magonjwa. Inasikitisha kuona kwamba, wawekezaji wengi Barani Afrika wanataka kujinufaisha kwa kuchota rasilimali mbali mbali kwa ajili ya mafao yao, lakini Bara la Afrika linaendelea kubaki nyuma licha ya utajiri mkubwa uliopo.

Kuna haja ya kubadili mchakato wa ushirikiano wa kimataifa, kwa kuwekeza zaidi katika majiundo ya watu; kwa kuboresha elimu inayotolewa kwenye taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kupambana barabara na mazingira yao na hatimaye, kuyabadili, dunia iweze kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi.

Utamaduni wa mshikamano wa dhati, ndiyo changamoto kubwa kwa wakati huu ili kuweza kufikia Malengo mbali mbali yanayobainishwa na Jumuiya ya Kimataifa, si tu yale yaliyotajwa kunako mwaka 2000, bali hata yale yanayoendelea kujitokeza katika maisha ya mwanadamu kwa wakati huu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.