Askofu mkuu mstaafu Alessandro Plotti wa Jimbo kuu la Pisa, Italia katika maadhimisho
ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari 2015, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu
Yohane, lililoko mjini Roma, ametoa Darala la Ushemasi kwa Wamissionari wawili wa
Mapendo, maarufu kama Warosimini.
Mashemasi
hawa ni Aristid Shayo kutoka Tanzania na Shemasi Justus Okibo kutoka Kenya. Katika
Ibada hii ya Misa Takatifu, Askofu mkuu mstaafu Plotti amefanya pia kumbu kumbu ya
miaka 34 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu.
Katika mahubiri yake Askofu mkuu
mstaafu Plotti amekazia umuhimu wa Umissionari unaomwilishwa katika huduma ya mapendo;
huduma kwa Neno la Mungu, linalotamadunishwa katika uhalisia wa maisha ya watu sanjari
na kujikita kwa njia ya sala na tafakari kuitafuta ile nyota angavu, yaani Yesu Kristo
katika kuishirikisha Familia ya Mungu mwanga wa upendo na huruma ya Mungu.
Baadhi
ya waamini ndani ya Kanisa Katoliki kwa kuwekewa mikono na Askofu wanapewa Daraja
la Ushemasi, wakiwa na dhamana na utume wa kuhudumia Altareni, Kuhubiri Neno la Mungu,
kuwagawia waamini Ekaristi Takatifu, kuhudumia wakati wa mazishi na kusaidia kuendesha
Ibada mbali mbali kadiri ya Daraja la Ushemasi pamoja na kutambua kwamba, Mashemasi
ni wahudumu wakuu wa matendo ya huruma yanayofanywa na Mama Kanisa kwa waja wake.
Mashemasi wanapaswa kutambua kwamba, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa
jamii ni hazina na utajiri mkubwa wa Mama Kanisa katika maisha na utume wake.
Askofu
mkuu Plotti katika utangulizi wa Ibada ya Misa anasema, Siku kuu ya Epifania ni tukio
linalomwonesha Yesu, Mwanga wa Mungu akijifunua kwa Mataifa na utukufu wake ukaonekana
mjini Bethlehemu, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumfungulia
malango ya mioyo yao, ili Kristo Mwanga wa mataifa apate kuingia na kuwaangazia katika
mapito, maisha na historia yao. Mashemasi wapya waongozwe na mwanga huu kwa kuendelea
kuchota utajiri kutoka kwa Mwenyeheri Rosmini, Mwanzilishi wa Shirika la Mapendo ili
kuwahudumia Watu wa Mungu kwa ari na moyo mkuu!
Askofu Plotti katika mahubiri
yake, amewataka Mashemasi wapya, kuhakikisha kwamba, wanatoa huduma ya upendo kwa
maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kutambua kwamba, maskini ni
hazina kubwa kwa Mama Kanisa na kwamba, Yesu hakuzaliwa kwenye majumba ya Kifalme,
bali alizaliwa katika pango ya kulishia wanyama, yaani alizaliwa katika hali ya umaskini,
kule mjini Bethlehemu, lakini hata hivyo bado aliendelea kuwa na mvuto pamoja na mashiko
kwa wachungaji waliokuwa wanalisha wanyama wao kondeni, kama ilivyokuwa pia kwa Mamajusi
kutoka Mashariki ya Mbali.
Ujumbe wa Habari Njema, unajikita katika maneno
yanayoleta changamoto na bashasha katika maisha ya waamini! Simama, tazama, angaza,
amezaliwa Mkombozi wa dunia, nyota angavu. Hapa swali la msingi ambalo mwamini anapaswa
kujiuliza ni kama ikiwa yuko tayari kuupokea mwanga unaokuja! Je, ametoa kipaumbele
cha kwanza kwa uwepo wa Kristo katika maisha. Wakristo wanapaswa kuwa macho na makini,
ili kushinda kishawishi cha kukata tamaa au kukatishana tamaa, vikwazo katika mchakato
wa kutaka kumwona Mtoto Yesu.
Askofu mkuu mstaafu amewakumbusha Waamini kwamba,
hija iliyofanywa na Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali ni sawa na hija ya maisha ya
kiroho inayofanywa na kila mwamini; hija inayojikita katika uaminifu, udumifu, daima
wakiwa na taa zinazowaka na akiba ya mafuta, ili kufanikisha mchakato wa kumtafuta
Mtoto Yesu, Fumbo lililokuwa limefichika tangu milele, lakini watu wa nyakati hizi
wamepata bahati ya kufunuliwa Fumbo hili. Changamoto kwa waamini kuwa macho, kuendelea
kusali na kumpatia Mungu kipaumbele cha kwanza, ili aweze kuwaongoza katika hija ya
maisha ya hapa duniani sanjari na kuandika historia katika maisha yao.
Askofu
mkuu mstaafu Plotti amewataka Mashemasi na waamini katika ujumla wao kuhakikisha kwamba,
daima Mwenyezi Mungu anapowatembelea akute malango ya maisha yao yakiwa wazi, kwa
kuwamegea wengine furaha inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu; sanjari
na kujenga umoja na mshikamano katika kuwahudumia watu wa Mungu.
Epifania
ni Siku kuu ya Kristo anayejionesha miongoni mwa mataifa, ni siku kuu ya Kanisa la
Kiulimwengu, lakini kwa bahati mbaya hata leo hii bado kuna akina Herode wanaotaka
kujihudumia wenyewe badala ya kuhudumia Kanisa; huu ni uwili ambao unajitokeza hata
ndani ya Kanisa kutokana na uwepo wa dhambi miongoni mwa watoto wa Kanisa wanaochuchumilia
utakatifu wa maisha. Mashemasi wanachangamotishwa kuendeleza huduma katika mapendo
na kwamba, ushemasi ni huduma ya kudumu hata baada ya kupokea Daraja Takatifu la Upadre.
Wakleri wanapaswa kuendelea kutoa huduma ya huruma, mapendo na msamaha kwa ajili ya
Watoto wa Mungu.
Askofu mkuu Plotti amewataka Mashemasi wapya kuwa ni Wamissionari
na wahudumu wa Neno kwa kulimwilisha na kulitamadunisha katika maisha na mazingira
ya watu, ili watu waweze kuona mwanga na kutoka gizani, ili kuonja upya wa maisha
unaobubujika kutoka katika Neno la Mungu. Watu wana kiu kubwa ya kutaka kusikia Neno
la Mungu.
Yesu Kristo ndiye Mkombozi wa kweli aliyekuja kumwokoa mwanadamu
kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kumstahilishia binadamu kuitwa mwana
mpendwa wa Mungu. Vita na kinzani haviwezi kumkomboa mwanadamu katika shida na mahangaiko
yake, bali vitaendelea kusababisha majanga kwa watu na mali zao. Yesu Kristo ndiye
mwanga unaokoa na kuwawezesha watu kuwa ni Wamissionari, ili kuwatangazia jirani zao
Habari Njema ya Wokovu, kwa njia ya karama ya Shirika la Mapendo, ili kweli watu waweze
kuona na kuonja mabadiliko yaliyoletwa na Yesu Kristo.
Askofu mkuu mstaafu
Alessandro Plotti anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili
ya kuombea: amani, upendo, mshikamano; furaha ya kweli inayopata chimbuko lake kwa
Kristo; ili hatimaye, wao pia waweze kuwashirikisha wengine furaha hii.
Askofu
mkuu mstaafu anakiri kwamba, Upadre ni daraja linalobaliana na changamoto, matatizo
na magumu mbali mbali, lakini Wakleri wanapaswa kujifunza kutoka kwa Kristo ambaye
ni mpole na mnyenyekevu wa moyo na kwamba, mzigo wake ni mwepesi. Ile hamu na kiu
ya watu kutaka kukutana na Yesu ipate jibu makini kwa kukutana na wahudumu wa Injili,
ambao ni wakweli, wanyofu na watoto wapendwa wa Mungu.
Askofu mkuu mstaafu
pamoja na kuwa na umri mkubwa, umati wa Familia ya Mungu kutoka Afrika Mashariki,
Italia na nje ya Italia, wamemkubali kwa "kushusha ndondo za uhakika", kielelezo kwamba,
"amekula nchumvi nyingi" katika maisha na huduma ya Kipadre.
Na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya radio Vatican.