2015-01-07 14:22:58

Vijana kutoka Niger wanajiunga kwa wingi na Boko Haram!


Askofu mkuu Michel Cartatèguy wa Jimbo kuu la Niamey, Niger anasema, kuna idadi kubwa ya vijana kutoka nchini Niger wanaojiunga na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram, katika mkoa wa Diffa, ambao uko mpakani na Nigeria, jambo ambalo ni hatari kabisa kwa usalama wa raia na mali zao! Vijana kutoka mkoa wa Diffa wanaendelea kujiandikisha na kupewa mazoezi ya kuwa ni wanachama wa Boko Haram, kikundi ambacho hadi sasa limekuwa ni chanzo cha majanga na maafa makubwa Nigeria na katika nchi jirani!

Boko Haram imekwisha kuteka ngome ya Baga, iliyokuwa inatumiwa na majeshi ya Nigeria, Chad, Niger na Cameroon, hali ambayo inaendelea kusababisha hofu na wasi wasi mkubwa kwa ajili ya amani katika maeneo yaliyoko Kaskazini Mashariki mwa Nigeria. Mkoa wa Diffa unakadiriwa kuwa na wakimbizi wapatao 150, 000 kutoka Nigeria ambao wanahifadhiwa katika eneo hili. Ni kundi la watu ambalo limelazimika kuacha makazi yake, ili kusalimisha maisha.

Askofu mkuu Michel Cartatèguy anasema mkoa wa Diffa ni kati ya maeneo maskini sana nchini Niger, lakini hata katika umaskini wake, watu wanaendelea kuonesha upendo na ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Nigeria wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Anasema, inasikitisha kuona kwamba, vyombo vya habari kitaifa na kimataifa havilipatii uzito unaostahili, tatizo la uwepo wa Boko Haram mkoani hapo!







All the contents on this site are copyrighted ©.