2015-01-07 10:04:00

Mchapo!


Katika fasihi andishi kuna mitindo mingi ya kuandika habari. Kuna ushahiri, tamthilia, hadithi nk. Leo tutakutana na mtindo mpya kabisa wa uandishi tunaoweza kuuita, “Mtindo wa Safari,” Mwandishi amemwandika binadamu akiwa katika safari ya maisha hapa duniani.

Binadamu huyo ni Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliyezaliwa kwetu. Yesu anaanza safari ya maisha yake ya hadharani kama mwalimu. Kabla ya kuanza kufundisha alimbidi kusafiri kutoka Galilea hadi Yudea ili kubatizwa. Baada ya kubatizwa na Yohane kwenye mto Yordani, ndipo anaanza safari ya kufundisha akiwa na mitume wake. Miaka mitatu ya kufundisha, ilikuwa ni fursa pekee kwa Yesu ya kudhihirisha uso wa Mungu, hali yake, mafundisho yake, mapendekezo yake, rai zake, na sera zake. Mbele ya rai hizo kila mmoja alikuwa na uhuru wote wa kuchagua kumfuata au la.

Hata wewe ndugu yangu, maisha yako hapa duniani ni kama safari. Mwinjili anatualika wasomaji wake wote kutembea na Yesu, kumtafakari huyu mwalimu na kusikiliza ujumbe wake, kadhalika anatualikwa kuutafakari uso wa Mungu uliojidhihirisha katika Mwanae Yesu Kristo.

Marko hasimulii matukio ya kuzaliwa Yesu kama wanavyofanya wainjili Luka na Mateo, yeye anaanza mara moja na ubatizo wa Yohane. Anaanza na maneno ya Yohane Mbatizaji: “Mimi ninawabatiza kwa maji, bali yeye atawabatiza katika Roho Mtakatifu.” Yohane aliyasema maneno hayo akiwa karibu na bahari ya chumvi, pale ambapo mto Yordani unaingia baharini. Mto Yordani ni muhimu sana kwa wayahudi kwani ulikuwa ni mpaka kati ya nchi ya wapagani yaani utumwani, na nchi huru ya wayahudi. Wakati huo, Yohane Mbatizaji, alikuwa upande wa nchi ya wapagani, pahala ambapo Yoshua alivuka na watu wake toka utumwani Misri na kuingia nchi ya ahadi.

Yohane Mbatizaji alihubiri kwamba, hiyo nchi waliyoingia kabla wakiongozwa na Yoshua haikuwa nchi huru hata kama ilikuwa ya ahadi. Kwa hiyo sasa alihitajika Yoshua mpya atakayewaongoza katika nchi huru ya ahadi ambaye ni Yesu Kristo mwenyewe. Yesu anapojitokeza, Yohane Mbatizaji anakiri kwamba ubatizo wake ni tofauti na ule wa Yesu. Kwamba ubatizo wake Yohane ni alama tu ya nje, inatakiwa ubatizo mwingine unaomwongoza mtu kuishi akiongozwa na mtu. Ndiyo maana anasema kuwa Yesu atabatiza kwa Roho mtakatifu. Roho huyo ni nguvu ya ndani isiyoonekana kwa nje, na inaletwa na nafsi ya Yesu inayomfanya mtu kuwa huru.

Baada ya kueleza tofauti hizi za ubatizo, anaielezea safari ya Yesu hadi kufika pale Yordani. Yesu aliondoka Nazareti kule Galilea. Badala ya kukatisha katikati ya Samaria na kufika Yerusalemu, akapita Esdra kisha akavuka Mto Yordani hadi mashariki, nchi ya wapagani, na kuambaa pembeni ya mto Yordani kuelekea kusini hadi Betbara, karibu na pahala mto unapoingia baharini. Bethbara maana yake mahali pa kuangalia, pale ambapo Moses alisimama na kuangalia nchi ya ahadi. Hapo ndipo alipokuwa Yohane akibatiza.

Mto Yordani unapoingia baharini unaonekana umebeba matope, udongo na dinga iliyoshonana. Wakati wa ubatizo Yesu aliingia ndani ya mto huo akabatizwa na kuvuka kuelekea upande wa nchi ya ahadi. Tendo la Yesu kuingia ndani ya jito hilo lenye tope, ni alama ya kuchukua hali halisi ya utope au udongo wa maisha yetu. Binadamu tumefanywa kwa udongo, uliopuliziwa roho ya uhai na uzima wa kimungu. “Alipopanda kutoka majini” vikatokea vituko vitatu. Mosi, Mbingu zilipasuka. Pili, Roho kama hua alishuka juu ya Yesu. Tatu, Sauti ikatoka mbinguni.

Kituko cha kwanza ni kupasuka mbingu. Katika fikra za Wayahudi, kulikuwa na mbingu saba zilizojipanga moja juu ya nyingine. Mungu mwenyewe alikaa mbingu ya mwisho. Ilikuwa inachukua miaka mia tano kusafiri kutoka mbingu moja hadi nyingine. Safari hiyo ilikuwa refu sana kwa binadamu. Ili kuwasiliana na binadamu Mungu ilimbidi awe anatuma Manabii, lakini hata hivyo, watu hawakuwasikiliza. Mapato yake Mungu alifunga mbingu yake na kuishi kivyake.

Kwa hiyo Waisraeli wakajisikia vibaya sana na walipokuwa utumwani Babeli wakasali: Bwana ulikuwa na haki ya kutukasirikia, maana tulitenda dhambi; Lakini sasa, Ee Bwana, wewe u baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu, sisi sote ni kazi ya mikono yako. Ukifungua mbingu tutaokoka”. (Isaya 63-64). Sasa mbingu zinapofunguka tena, mwinjili anatumia neno schizein maana yake kupasuka. Toka neno hilo tunapata schisma lenye maana ya mpasuko kama ule wa kanisa la mashariki na magharibi. Neno hilo Schizein, litatumika tena pale Yesu anapokufa, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili.

Kituko cha pili ni cha roho kama hua akamshukia kama njiwa. Roho maana yake ni nguvu, au uwezo wa kupenda bila masherti, kutolea kabisa nguvu ya maisha aliyopata toka kwa Mungu. Picha ya kwanza ya njiwa inaturudisha kwa roho yule aliyekuwa ametanda juu ya uso wa maji kabla ya uumbaji wa ulimwengu. Leo njiwa anafika tena kuonesha mwanzo wa uumbaji mpya, uumbaji wa binadamu anayepokea uzima wa Kimungu.

Picha ya pili ya njiwa inaturudisha wakati wa Nuhu. Jioni moja baada ya mafuriko njiwa alirudi kwenye safina akiwa na tawi la mizeituni mdomoni kuashiria amani, utulivu. Sasa kwa njia ya roho wa Yesu tunapata tena amani. “utukufu kwa Mungu juu, na amani duniani kwa watu anaowapenda”.

Picha ya tatu ya njiwa ni ile tabia yake ya kutafuta kiota chake. Hapa Roho ya Baba anamtafuta Yesu Kristo kama kiota chake pekee anakoweza kutulia, kuishi na kujikamilisha. Picha ya nne ya njiwa ni ile hali yake ya wororo, ya uzuri, ya ulaini inayowakilisha upendo na huruma. Nguvu ya roho hiyo ndiyo inayombadilisha mtu na siyo nguvu ya mabavu, bali nguvu ya upendo, ya ulaini na ya utulivu. Roho huyo ndiye atakayewakusanya wote na kuwatatuliza, atatangaza uhuru kwa wote wanaokandamizwa. Roho huyo tumepewa hata sisi siku ya ubatizo na kipaimara inabidi ajioneshe katika matendo yetu ya wema na huruma.

Kituko cha tatu ni sauti toka mbinguni. Marabi walikuwa wanaonesha daima kwamba Mungu toka mbinguni aliyekuwa anamnadisha na kumthibitisha Yesu kwamba: “Wewe ni mwanangu” (Zaburi 2). Kadhalika mfalme alipokuwa anasimikwa madarakani, alitambuliwa pia na Mungu, na alitakiwa kuonesha picha ya Mungu hapa duniani.

Kwa sauti hiyo itokayo mbinguni Yesu asimikwa rasmi madarakani na Mungu mwenyewe na anatambulika kama Mwana wake mpendwa. Isieleweke kwamba alikuwa mtoto wa kimwili, la hasha, bali alikuwa anafanana na Mungu kwa kila kitu, kwani aliidhihirisha sura ya Mungu. Kwa hiyo sisi tunaweza kumtambua Mungu kwa njia ya huyu mwanae.

Tunaalikwa kumfuata Yesu katika safari ya maisha yake, tuitambue na kuitafakari sura ya Kristo ambayo Mungu Baba anaitambua. Safari yetu ya maisha iongozwe na roho wa Kristo ili sura yetu iweze kutambuliwa na Mungu. Nakutakia safari njema!

Padre Alcuin Nyirenda, OSB








All the contents on this site are copyrighted ©.