Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alisema, utakatifu ndiyo sura nzuri zaidi inayopendeza
machoni pa walimwengu, changamoto kwa Familia ya Mungu kuhakikisha kwamba, inajikita
katika utakatifu wa maisha, kila mtu kadiri ya wito, dhamana na karama yake katika
maisha na utume wa Kanisa.
Ikumbukwe kwamba, kila wito unafumbata uzuri na
changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi katika hija ya maisha ya kila siku kama sehemu
ya mchakato unaotafuta kumwilisha utakatifu wa maisha katika uhalisia wa maisha, Fumbo
la Utatu Mtakatifu, likipewa kipaumbele cha kwanza!
Ni changamoto ambayo imetolewa
hivi karibuni na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati alipokuwa
anashiriki kwenye kongamano la kitaifa kuhusu miito, lililoandaliwa na Baraza al Maaskofu
Katoliki Italia, kuanzia tarehe 3 hadi tarehe 5 Januari 2015. Katika mahubiri yake,
Kardinali Parolin amewataka waamini kutambua na kuguswa na uzuri huu wenye mvuto unaopania
kuwapatia mabadiliko makubwa katika maisha yao, kwa kukutana na Yesu katika Sakramenti,
Maandiko Matakatifu, lakini zaidi kati ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa jamii.
Kardinali Parolin anawauliza waamini swali msingi, ikiwa kama kweli
wameguswa na Maandiko Matakatifu, kiasi cha kuwachangamotisha kufanya mabadiliko msingi
katika maisha yao? Au bado wanaendelea kutangatanga bila ya kuwa na mwelekeo sahihi
wa maisha kama "dala dala iliyokatika usukani? Waamini wanapaswa kujenga imani yao
kwa Kristo na Kanisa lake, ili kweli wito na maisha yao yawe ni ushuhuda wa utakatifu
unaobubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe.
Kardinali Pietro Parolin anasema,
haitoshi kwa mwamini kuvutwa na kuguswa na uzuri pamoja na ukweli, lakini wanapaswa
kutambua umuhimu wa ujenzi wa mazingira ambamo mambo haya msingi yanaweza kumwilishwa
katika uhalisia wa maisha sanjari na kuwashirikisha wengine, pasi na kumezwa na ubinafsi
ambao kwa sasa ni kama ugonjwa unaomwandama mwanadamu. Waamini wakati huu wa Kipindi
cha Noeli, wamwangalie Mtoto Yesu alivyolazwa kwa unyenyekevu pale Pangoni, huku wakizungukwa
na usiku wa giza nene!
Watu wanahitaji kuona cheche za mwanga, ili kutambua
kwamba, wanazungukwa na giza nene! Utakatifu ni mwanga angavu katika maisha na utume
wa Kanisa, sura yenye mvuto na mashiko!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.