2015-01-06 10:23:26

Ustawi na hatima ya Afrika iko mikononi mwa Waafrika wenyewe!


Kardinali Thèodore Adrian Sarr, Askofu mstaafu wa Jimbo kuu la Dakar, Senegal anawataka Waafrika kuhakikisha kwamba, wanajifunga kibwebwe ili kuharakisha mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Bara la Afrika na kwamba hakuna tena mjomba anayeweza kuwatetea; kwa wale wanaofanya hivyo wengi wao wana ajenda za siri!

Wananchi Barani Afrika, katika mapambazuko ya karne ya ishirini na moja, hawana budi kushirikiana na kushikamana kwa dhati, huku wakijitahidi kuondokana na vita pamoja na kinzani zinazokwamisha mchakato wa maendeleo endelevu, kwa kujipangia mikakati ya maendeleo na kuhakikisha kwamba, inatekelezwa kwa ajili ya ustawi na mafao ya Bara la Afrika. Wananchi wa Bara la Afrika hawana budi kuhakikisha kwamba, mustakabali wa Afrika unawekwa mikononi mwao badala ya kuwaachia wageni na watu wachache wenye uchu wa mali na madaraka!

Kardinali Adrian Sarr, anawataka wananchi wa Bara la Afrika kuchakarika ili waweze kujiletea maendeleo endelevu badala ya kuwaachia baadhi ya watu kufanya maamuzi kwa niaba yao, kana kwamba wao hawana uwezo. Umefika wakati kwa Bara la Afrika na taasisi zake, kujadili, kupanga na kutekeleza mikakati kwa ajili ya maendeleo ya watu wake.

Kardinali Sarr ameyasema haya hivi karibuni alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Bodi ya Kitaifa dhidi ya uvutaji tumbaku nchini Senegal, (Listab). kardinali Sarr ni mjumbe wa heshima wa bodi hii kutokana na juhudi zake dhidi ya uvutaji wa tumbaku ambao umekuwa na madhara makubwa kwa afya za wananchi ndani na nje ya Senegal.

Kardinali Sarr anasema, kuna haja ya kutengeneza sheria itakayopiga rufuku matumizi ya tumbaku ambayo yana madhara makubwa kwa watu, licha ya kuwa ni chanzo kikuu cha kodi kwa Serikali mbali mbali.







All the contents on this site are copyrighted ©.